Kwa mara ya kwanza tangu kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad miezi 19 iliyopita, vikosi vya jeshi la Iran vimeshambulia kwa njia ya anga eneo lililo ndani ya ardhi ya Syria.

Idara ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ilitangaza katika taarifa siku ya Ijumaa, Julai 17 kwamba: Ikiwa ni katika kujibu vitendo vya kikatili vilivyofanywa karibuni na jeshi linaloua watoto la Marekani, wapiganaji wa Kikosi cha Anga cha IRGC wametekeleza wimbi la kumi na moja la Operesheni ya Nasr-2. Katika operesheni hiyo iliyotekelezwa kwa ajili ya kulipiza kisasi cha askari waliodhulumiwa na kuuawa shahidi huko Bampur, Iranshahr, wapiganaji hao wamefanya shambulio la kushtukiza dhidi ya kituo cha kamandi ya operesheni maalum cha adui katika eneo la Al-Tanf nchini Syria, ambapo mbali na kuharibu mfumo wa rada na helikopta kadhaa maalum za operesheni katika kituo hicho, wamewaangamiza na kuwapeleka kuzimu idadi kubwa ya askari wetendajinai wa Marekani.

Vyanzo vya Syria vimethibitisha shambulio hilo dhidi ya kambi ya Marekani huko Al-Tanf, huku upande wa Marekani ukikanusha kutokea kwa vifo au majeraha, au kudai kuwa yalikuwa madogo. Hili ni shambulio la kwanza kuwahi kufanywa na Iran dhidi ya eneo la Marekani nchini Syria tangu kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad mnamo Desemba 2024. Al-Tanf iko kusini-mashariki mwa Syria, karibu na mipaka ya Iraq na Jordan, na vikosi vya Marekani vilianzisha kambi katika eneo hilo mwaka 2016. Umbali kutoka mpaka wa Iran hadi Al-Tanf, Syria, ni takriban kilomita 800.

Ikumbukwe kuwa operesheni hii ilifanyika saa chache tu baada ya viongozi wa serikali ya mpito ya Syria kutangaza kukamatwa kwa shehena ya ndege zisizo na rubani (drones), wakidai kuwa zilikuwa zimefichwa ndani ya gari la kubebea mafuta lililokuwa limeingia nchini humo kutokea Iraq, likielekea katika mji wa Baniyas. Walidai kuwa ndege hizo zilikusudiwa kusafirishwa kwa siri kwenda kwa kundi la Hizbullah ya Lebanon, madai ambayo yalikanushwa vikali na Hizbullah, ikisisitiza kuwa haiendeshi shughuli zozote ndani ya ardhi ya Syria. Mbali na taathira za moja kwa moja za shambulio hilo ambalo IRGC ilitangaza kuwa ni sehemu ya wimbi la kumi na moja la “Operesheni ya Nasr-2,” iliyoanzishwa chini ya kaulimbiu ya “Ya Aba Abdillah al-Hussein”, shambulio hilo linatoa jumbe mbalimbali za kisiasa. Hili ni jambo muhimu hasa zikitiliwa maanani kauli za mara kwa mara za Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu serikali ya Syria inayoongozwa na al-Julani kwamba itahusika pakubwa katika vita dhidi ya Hizbullah ya Lebanon.

Ingawa shambulio dhidi ya kambi ya Al-Tanf limetekelezwa kama jibu la kutumwa vikosi vya Marekani katika eneo, lakini pia linaweza kutafsiriwa katika muktadha mpana zaidi unaohusisha watawala wa Syria moja kwa moja, na ndio maana hadi sasa wamenyamaza kimya bila kutoa jibu lolote. Kufikia sasa, inaonekana Syria imeamua kudumisha sera ya kutofungamana na upande wowote kuhusiana na mzozo unaoendelea kati ya Iran na Marekani. Operesheni ya Iran iliyolenga kambi ya Marekani huko Al-Tanf, Syria, imetoa jumbe kadhaa za kimkakati kwa Marekani na washirika wake.

Ujumbe wa kwanza ni onyo dhidi ya mipango au mahesabu yoyote ya kimakosa yanayolenga kuifanya Syria kuwa eneo la kuanzishia vitendo vya kichokozi dhidi ya Hizbullah. Kwa mujibu wa wataalamu, shambulio dhidi ya Al-Tanf limebainisha wazi mipaka ya nafasi yoyote ambayo Syria inaweza kuwa nayo katika hali kama hiyo. Ujumbe wa pili unaelekezwa kwa Jordan. Kwa mujibu wa uchambuzi huu, iwapo wigo wa mgogoro huo utapanuka, kambi zote za kijeshi za Marekani katika eneo hilo, iwapo zitatumika kusaidia operesheni za kijeshi, zitakuwa sehemu ya uwanja wa vita.

Ujumbe wa tatu unaelekezwa moja kwa moja kwa Washington yenyewe. Shambulio la Iran dhidi ya Al-Tanf, eneo lililoko kwenye makutano ya mipaka ya Syria, Jordan, na Iraq, linaonyesha kuwa iwapo vita vitaendelea na kuongezeka makali, mgogoro huo unaweza kuvuka mipaka ya Ghuba ya Uajemi na kuenea katika pembeze zote ambapo vikosi vya Marekani vimewekwa katika Asia Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *