Babati. Mkoa wa Manyara unalenga kukusanya Sh1.5 bilioni kupitia mbio za Manyara Tanzanite Marathon, zitakazotumika kujenga jengo la mama na mtoto pamoja na kuboresha huduma za watoto wachanga na njiti, hatua inayolenga kuokoa maisha ya maelfu ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kila mwaka.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema takribani watoto njiti 3,000 huzaliwa kila mwaka katika wilaya za Hanang’, Kiteto, Simanjiro, Mbulu na Babati, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha huduma za afya kwa kundi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati leo Jumanne Julai 21, 2026, Sendiga amesema fedha hizo zinatarajiwa kupatikana kupitia mbio za Manyara Tanzanite Marathon, zitakazofanyika Agosti 22, 2026, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.

Mbio hizo zitafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto” na zinatarajiwa kuwashirikisha wanariadha wa kimataifa pamoja na washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini.

“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki na kuchangia. Tunataka kuona watoto wanaozaliwa njiti wanapata huduma bora, wakue salama na baadaye wawe wanariadha, viongozi na wataalamu watakaolitumikia Taifa,” amesema Sendiga.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Roghat John Akhwari amesema mbio hizo zitakuwa fursa ya kuitangaza zaidi Manyara na kuhamasisha maendeleo ya riadha nchini.

Amesema shirikisho linakusudia kuziingiza mbio hizo katika kalenda yake rasmi ili ziwe zikifanyika kila mwaka kwa lengo la kuchangia huduma za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Andrew Method amesema fedha zitakazopatikana zitatumika kujenga jengo la mama na mtoto pamoja na kununua vifaatiba muhimu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wachanga na njiti.

Mwanariadha wa kimataifa kutoka Kata ya Madunga wilayani Babati, Gabriel Geay amesema mbio hizo zitakuwa na manufaa zaidi ya kuchangisha fedha, kwani pia zitasaidia kuibua vipaji vipya vya riadha na kuwapa vijana fursa ya kufikia mafanikio kupitia mchezo huo.

Naye mkazi wa Mtaa wa Oysterbay mjini Babati, Neema Tsakara amewataka wakazi wa Manyara kujitokeza kwa wingi kuunga mkono kampeni hiyo kwa kuchangia ili kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga na njiti.

“Tunapaswa kumuunga mkono mkuu wetu wa mkoa katika jitihada hizi. Michango yetu itasaidia kuokoa maisha ya watoto wengi na kuboresha huduma za afya kwa vizazi vijavyo,” amesema Neema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *