Mvutano ndani ya CHADEMA umechukua sura mpya baada ya viongozi watatu wa chama kutoka Morogoro na Tanga kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, wakipinga hatua zilizochukuliwa dhidi yao walipopaza sauti kuhusiana na tuhuma za ubadhirifu wa pesa za michango ya wadau kwa chama hicho unaodaiwa kufanywa na makamu mwenyekiti wao John Heche na kudai zilikiuka Katiba na Kanuni za chama .
Viongozi hao ni Barnabas Okola, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Morogoro, Mathias Cosmas, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Kilindi, na Joseph Mwakidasi, Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Muheza.
Katika taarifa yao kwa umma ya Julai 21, 2026, wamesema hawakupewa taarifa rasmi za tuhuma zinazowakabili, hawakuitwa kusikilizwa wala kupewa nafasi ya kujitetea kabla ya maamuzi yaliyotangazwa.
Wamedai kuwa hatua zilizochukuliwa dhidi yao ni batili kwa kuwa hazikufuata utaratibu uliowekwa na Katiba na Kanuni za CHADEMA, hivyo bado wao ni viongozi halali wa chama hadi taratibu za kikatiba zitakapokamilika.
Kupitia barua yao, viongozi hao wameiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutumia mamlaka yake kuhakikisha Katiba na Kanuni za CHADEMA zinazingatiwa, kuchunguza madai ya ukiukwaji wa taratibu za ndani ya chama na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Hatua hiyo inaongeza orodha ya migogoro ya ndani ya CHADEMA inayofikishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, huku ikitarajiwa kufungua mjadala mpya kuhusu ufuataji wa taratibu za kikatiba ndani ya chama hicho.
Jitihada za kumpata Msajili wa Vyama vya Siasa ili kuzungumzia malalamiko hayo na kueleza hatua zinazoweza kuchukuliwa zinaendelea.
(Feed generated with FetchRSS)