
Mkuu wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) wenye makao yake makuu huko Roma ameonya kuwa, migogoro na machafuko katika masoko ya nishati duniani vinaweza kuwasukuma mamilioni zaidi ya watu kwenye njaa kwa kuzidisha gharama za mafuta, mbolea na chakula. Taarifa hii imetolewa huku ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa ikionyesha kuwa maendeleo ya kimataifa dhidi ya njaa bado yako tete.
Ripoti ya usalama wa chakula ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana Jumanne, imegundua kuwa njaa duniani imepungua kwa kiasi katika miaka ya hivi karibuni, lakini imetabiri kwamba zaidi ya watu milioni 500 bado wanaweza kukabiliwa na njaa sugu ifikapo mwaka 2030.
Afrika inatabiriwa kubeba sehemu kubwa zaidi ya mzigo huo.
Katika mahojiano na The Associated Press mnamo Julai 10, Rais wa IFAD Alvaro Lario amesema kwamba mvutano wa kijiopolitiki na matatizo yanayoweza kujitokeza kwa meli na usambazaji wa nishati – ikiwa ni pamoja na kutokuwa na uhakika kuhusu Lango-Bahari la Hormuz kutokana na vita vya Marekani dhidi ya Iran – vinaweza kuwatumbukiza watu milioni 9 hadi 18 zaidi katika njaa ikiwa hali hii itaendelea.
Lario amesema migogoro inasalia kuwa mojawapo ya vikwazo vikubwa vya juhudi za kupunguza njaa duniani kote.
Amesema vita na mivutano ya kijiopolitiki vinaweza kuvuruga usafirishaji, usambazaji wa nishati na pembejeo za kilimo, na kuongeza gharama katika mifumo yote ya chakula ambayo tayari imeathiriwa na mfumuko wa bei.
Ameongeza kuwa bei kubwa za nishati tayari zinaathiri mbolea na uzalishaji wa kilimo.
Afisa huyo wa UN amesema mabadiliko ya tabianchi yanaongeza mashinikizo kwa mifumo ya chakula na riziki za vijijini.
Ripoti hiyo inaangazia Afrika kama changamoto kubwa zaidi ya usalama wa chakula duniani.
Kwa mara ya kwanza, bara hilo limeipiku Asia kama eneo lenye idadi kubwa zaidi ya watu wenye njaa, na karibu asilimia 60 ya watu wenye utapiamlo sugu duniani wanaweza kuwa barani Afrika ifikapo mwaka wa 2030.
Alvaro Lario amehusisha mabadiliko hayo kwa kiasi fulani na ukuaji wa haraka wa idadi ya watu na faida za kiuchumi zinazopungua polepole kuliko katika sehemu za Asia, na ametaka kufanyike uwekezaji mkubwa katika kilimo, miundombinu na mifumo ya chakula barani Afrika.