Rais wa Cameroon, Paul Biya, mmoja wa marais waliokaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, hajaonekana nchini humo kwa zaidi ya mwezi mmoja hali hii ikiibua mjadala kuhusu afya yake na mrithi wake ikizingatiwa kuwa hakuna makamu wa rais.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kufikia Julai 21, ni siku arobaini na tano baada ya Biya kuondoka Cameroon kwa kile kilichoelezewa kama ziara fupi ya kibinafsi barani Ulaya, na kutorejea kwake kumeongeza uvumi kuhusu afya yake, mapendekezo yakitolewa kuwa wadhifa wa urais utangazwe kuwa wazi.
Chama cha upinzani cha UDC kinasema kuwa kutokuwepo kwa muda mrefu kwa rais Biya, hakumaanishi moja kwa moja kuwa kuna pengo, lakini kinahoji kuwa hali hiyo inazua maswali ya msingi kuhusu mwendelezo wa serikali na utekelezaji wa mamlaka ya urais.
Hata hivyo chama tawala cha RDPC kimepinga vikali tetesi hizi, kikisisitiza kuwa serikali inaendelea kufanya kazi.
Tangu Biya aondoke, akaunti rasmi za mitandao ya kijamii za rais zimeendelea kuchapisha ujumbe kutoka kwake, lakini, hakujawa na tukio lolote la rais kuonekana hadharani wala taarifa yoyote ya moja kwa moja kutoka kwake binafsi.
Wachambuzi wanasema Baraza la Katiba linapaswa kuchukua hatua baada ya siku 45, japokuwa hakuna sheria inayoweka kikomo wazi cha muda ambao rais anaweza kukaa nje ya nchi.