Juzi, nilifanya ziara ya kikazi iliyoishia kuwa ya kisasi na visasi kwenye kaya moja ya kufikirika kutokana na maajabu na mauzauza niliyoambiwa na kushuhudia pale wadudu walivyothamini hadi mafyatu wa huko ima kujigeuza au kugeuzwa wadudu na si vinginevyo. Nilishangaa na kuvutiwa na sera zake za ajabu. Nani angeamini kuwa mafyatu wazima wangeacha ufyatu na kuanzisha sera ya ududu wakitenda madudu kama wadudu au tuseme kuliko wadudu?

Nikiwa nashangaashangaa utadhani nilikuwa feri, si ikabidi niulize tena kiftyatu ili kujua kwanini kaya hii ambayo wengi huiita ya mazwazwa kuanzisha na kutumia sera ya ududu na si ufyatu.

Ndiposa mwenyeji wangu rahis wa kaya ya kufikirika ya Tazamia Bwana Nkubwa Sina Haya wala Sijali akaniibia siri kuwa wadudu ni wachafu, hivyo hawawezi kuhisi, kuona, wala kufichua uchafu wa awafugaye.

Kwenye sera ya ududu, uchafu hugeuzwa usafi na usafi uchafu. Sera hii inamruhusu mwenye kuitumia kuwahimiza wengine kufanya asiyofanya ndiyo maana huitwa unafiki kama siyo usanii na uzwazwa.

Hayo tuyaache. Ni ya fyatu wa kule na wadudufyatu wake na sera zao za uchafu, ududu, unafiki, na uzwazwa.

Baada ya kukamilisha ziara nikiwa nimeshanga si nikarejea Fyatuland na kulikoroga kwa kuwapasha kila kitu nisjue nilikuwa nawafyatua wanifyatue bila kujua! Mafytu wangu si wakaanza wamenishitakia. Waliwashitaki mafyatu wanene waliokuwa wakiwasisitiza walipe kodi wakati wao hawalipi. Wapo wanafiki na mashakunaku waliowahimiza mafyatu kuwa waadilifu wakati wao walikuwa wachafu tena wa kunuka kuliko hata wadudu japo hatuna sera ya ududu.

Wengine eti walikuwa wakiwahimiza mafyatu wawe wakweli wakati wao ni waongo wa kutupwa!

Sikjua kuwa kumbe mafyatu wanajua mambo mengi ila hawataki kufyatuka na kutufyatua sisi tunaowafyatua! Baada ya kuwasikiliza na kuwafunga kamba si nilijitoa ufahamu na kuunda duara la maoni.

We! Siku ya kukutana na kutoa nyongo yupo aliyenifyatua na kuniacha hoi. Ni pale nilipopendekeza kuwa na bajeti ya watoa habari za ufisadi, wizi, ujambazi, uvivu, uchawi, unafiki na mengine mengi kama hayo.

Bila hata kuona aibu, si lisema kuwa wengi wa tunaofanya haya mambo tunayokataza ni sisi wanene wenyewe. Hakuna kitu kiliniudhi kama Fyatu huyu kudai kuwa sisi ni waroho, tuna roho mbaya, walafi tulao kwa mikono na miguu tena bila kunawa.

Alienda mbali na kutufananisha na mainzi yalayo kwenye chombo na kutapika na kunihino humo huku yakiwatukana na kuwapigia kelele wenye vyao yalivilayo!

Kuna mwingine ambaye kwa ufyatu hata mie rahis wa Mafyatu simpati. Aliniangalia nilivyojaza mbele na nyuma na kusema kuwa tumbo langu limejaa haramu!

Akiwa hajamaliza, si nikamsikia mwingine akinong’ona kuwa mie ni mchawi na mnafiki ninayejifanya mtakatifu wakati ni mtakakitu tu.

Baada ya kuyadaka yote haya, sasa rasmi, natangaza sera ya uchawi, unafiki, usanii, na urongo ili kuwa mkweli katika kuitawala Fyatuland.

Mie siyo mnafiki ndiyo maana nataka sera hizo hapo juu zirasimishwe na Mafyatu wajue kuliko kuwageuza mazwazwa au wadudu. Kwa wasioniju vizuri wajue.

Nimesoma madude mengi ya kichawi kama vile Al-Ajnas, Al Awfaq, Al-Jawahir al-Lamma’a, Kitab al-‘uyun wa’l-hada’iq fi akhbar al-haqa’iq, Shams al-Ma’arif, au Kitab al Bulhan, na mengine mengi ya uchawi wa kimanga. Ngoja haya madude niyaachie hapa. Ila mjue, uchawi wangu siyo wa kimatumbi wala kingazija.

Natangaza rasmi. Kuanzia leo, mnafiki yeyote atakayejifanya fyatu mwema, namrogea mbali. Mchafu yeyote atakayetaka aonekana msafi ajue anaingia kwenye anga zangu.

Sitaki uongo wala uungufyatu bali ukweli na uwazi. Heri mafyatu wanichukie kwa ukweli wangu kuliko kunipenda kwa uongo wangu. Heri wanilaumu hata kwa wema wangu kuliko kunisifia kwa uovu na ukatili wangu.

Heri waning’ong’e tena wazi wazi kuliko kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa kama vile mie ni bonzo au zwazwa wakati ni bonge la mjanja tena professa emeritus asiye na matusi wala ambaye sikuzawadiwa, kupewa, wala kununua kama niliowaona kule kwenye kaya ya Tazamia ambayo unaweza kutazamia iwe bonge la kaya wakati imegeuzwa jamhuri ya ndizi aka banana republic.

Kuanzia leo, wateule wangu wote wanapaswa kutekeleza sera hii takatifu inayolenga kuua uongo, usanii, uzwazwa, ududu, na mazambe mengine mengi. Kuanzia leo, kila mteule wangu lazima aseme amaanishacho na kumaanisha asemacho na si vinginevyo.

Lazima wote wahubiri maji na kunywa maji na siyo mvinyo kama nilivyoona kule nilikokuwa ziarani juzi.

Kwa vile moja ya sera zangu mpya ni uchawi, nakaribisha wachawi wote waje niwape vyeo. Wanafiki kadhalika ili wezi sitaki vinginevyo watangaze wazi kuwa ni wezi na siyo wachukuaji wanaojifanya wawekaji wakati ni wezi na makuadi wao wanaouza mafyatu wa kule nilikokuwa ziarani.

Nimalize. Wanafiki wote watakaokuwa tayari kujitangaza waje niwape ulaji tufaidi pamoja. Hivi nimesemaje? Kumbe niko Mirembe!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *