
Dar es Salaam. Sehemu hii ya tatu ya simulizi ya familia ya mfanyabiashara Johan Harald Abrahamsson kuondolewa katika nyumba ya makazi yake yenye thamani ya Sh2.5 bilioni, iliyopigwa mnada kutokana na mkopo wa Sh10 milioni alioudhamini, utata wa hali ya umiliki wa sasa wa nyumba hiyo.
Nyumba hiyo iliyoko kitalu namb16, Jangwani Beach wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, ilipigwa mnada na benki ya Exim Bank (Tanzania) Limited, kwa amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara mwaka 2017 kufidia deni la mkopo huo.
Takribani miaka tisa Abrahamsson amekuwa akipambana mahakamani bila mafanikio na sasa amefungua tena shauri la maombi mchanganyiko ya kibiashara namba 8901/2026 akipinga mchakato wa utekelezaji wa amri ya mahakama hiyo.
Wajibu maombi katika shauri hilo ni Exim Bank, kampuni ya Dascar Limited (mdhaminiwa wa mkopo), dalali wa Mahakama aliyeendesha mnada huo, Mas & Associates Company Limited and Court Broker na mnunuzi, Yusuph Shabani Matimbwa.
Abrahamsson anadai kuwa amri ya ukamataji na kupiga mnada nyumba hiyo ilipatikana kwa njia za udanganyifu na kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, madai na tuhuma ambazo zimekanushwa na Exim na Matimbwa, huku Exim ikiibua pingamizi la awali.
Wakati kumbukumbu za Mahakama zikionesha kuwa nyumba hiyo ilishabadilishwa umiliki kutoka kwa Abrahamsson na kwenda kwa Shabani Matimbwa anayedaiwa kuinunua, taarifa za Wizara ya Ardhi mpaka Julai 2026 zinaonesha kuwa haijawahi kubadilishwa umiliki bali bado inamilikiwa na Abrahamsson.
Kumbukumbu hizo za mahakama zinaonesha kuwa Julai 3, 2018, Matimbwa alimwandikia Msajili Msaidizi wa Hati maombi ya uhamisho wa umiliki wa nyumba hiyo, akiomba isajiliwe kwa jina lake.
Julai 25, 2018 Jacquiline aliweka pingamizi dhidi ya hati hiyo kufanyiwa mabadiliko yoyote, na Agosti 30, 2018, Abrahamsson pia kupitia wakili wake kampuni ya Legal Link Attorneys alimwandikia msajili akiomba kusimamisha mchakato wa uhamishaji umiliki huo.
Katika barua hiyo alieleza mchakato wa uuzwaji wa nyumba hiyo umepingwa Mahakama ya Rufani na kwenye kesi ya ardhi aliyokua ameifungua mke wa Abrahamsson, Jacquiline Kweka Abrahamsson.
Hivyo walimuomba msajili kusimamisha mchakato wa uhamishaji umiliki huo kusubiri uamuzi wa mashauri hayo yote.
Hata hivyo, nakala kivuli ya hati ya nyumba hiyo ambayo Mwananchi limeiona inaonesha umiliki wa nyumba hiyo ulishahamishwa kutoka kwa Abrahamsson kwenda kwa Matimbwa, tangu mwaka 2018.
Mabadiliko hayo yameelezewa pia na Matimbwa mwenyewe katika hati yake ya majibu ya madai ya shauri la maombi lililofunguliwa na Abrahamsson.
Katika majibu hayo anaelezea mchakato wa ununuzi wa nyumba hiyo mpaka maombi hayo ya kubadilishwa umiliki kutoka kwa Abrahamsson kwenda kwake na kwamba mabadiliko hayo yalifanyika tangu mwaka 2018.
Katika shauri lingine lililofunguliwa na Abrahamsson kupinga mnada huo, Matimbwa amewasilisha hati mbalimbali za matokeo ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Msajili Msaidizi wa Hati zinazoonesha kuwa yeye ndiye mmiliki wa nyumba hiyo.
Miongoni mwa taarifa za upekuzi huo ni pamoja na ile ya Januari 2, 2019 na Januari 24,2019 zilizosainiwa na Msajili Msaidizi wa Hati, Juliana Ngonyani, ya Novemba 27, 2025 na Aprili 30, 2026 zilizosainiwa na Msajili Msaidizi wa Hati, Apollo Laizer.
Hata hivyo Wakati Matimbwa akitumia nyaraka hizo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ofisi ya Kanda ya Mashariki na ofisi ya Msajili wa Hati, upande wa Abrahamsson pia una nyaraka zinaonesha kuwa umiliki huo haujawahi kubadilishwa.
Kwanza, Machi 9, 2024 Jacquiline aliandika barua kwa Kamishna wa Ardhi, Kanda ya Dar es Salaam akiulizia hali ya umiliki wa nyumba hiyo iliyodaiwa kuuzwa na baadaye umiliki kuhamishiwa kwa Matimbwa.
Agosti 13, 2024 Kamishna katika barua iliyosaniwa kwa niaba yake na Johansen Chibanda alimjibu Jacquiline kuwa ofisi yake imefuatilia kwa kina katika ofisi ya Msajili wa Hati na kujiridhisha kuwa hakuna mabadiliko yaliyokwishafanyika bali mmiliki bado ni Johan Harald Chrsiter Abrahamsson.
Februari 2026 Jacquiline alifanya upekuzi rasmi (official search) na ripoti ya upekuzi huo
kuhusu hali ya umiliki wa nyumba hiyo iliyosainiwa na Msajili Msaidizi wa Hati, Kanda ya Dar es Salaam, Apollo Laizer, Februari 24, 2026 mmiliki bado ni Abrahamsson.
Pia ripoti hiyo ilionesha kuwa hati ya nyumba hiyo imewekwa rehani Exim Bank tangu Septemba 24, 2004, pia ina pingamizi (caveat) lililowekwa Februari 5, 2016 na Jacquiline Donath Kweka Abrahamsson.
Kwa mkanganyiko huo wa nyaraka za taarifa za hali ya umiliki huo kutoka ofisi moja, Mwananchi liliamua kufanya upekuzi ili kujiridhisha kuwa kati ya vielelezo vya pande hizo mbili ni upande upo uko sahihi.
Mtumishi wa ofisi hiyo aliyepokea maombi hayo alisema kuwa majibu yangepatikana ndani ya siku mbili na kwamba tutajulishwa.
Hata hivyo baada ya kupita zaidi ya siku saba, bila kupewa taarifa hiyo, Mwananchi lilionana na Msajili Msaidizi wa Hati, Apollo Laizer ambaye alisema kwamba mfumo ulikuwa bado haujahuishwa na kwamba kesho yake yatakuwa tayari.
Alipoulizwa kuhusu mkanganyiko wa taarifa za upekuzi wa umiliki wa nyumba hiyo alizonazo Matimbwa zikionesha kuwa ndiye mmiliki na alizo nazo Jacquiline Abrahamsson zinazoonyesha kuwa nyumba hiyo bado haijabadilishwa umiliki bali mmiliki bado ni Abrahamsso, alisema kuwa za Matimbwa ndizo halali.
Alipotakiwa kufafanua kauli hiyo alisema kuwa mabadiliko ya umiliki wa nyumba hiyo yalishafanyika kwenye jalada halisi, isipokuwa kwenye mfumo ndiko walikuwa bado hawajafanya mabadiliko.
Kuhusu hati ya nyumba hiyo kuwekewa pingamizi isifanyiwe mabadiliko yoyote, Apollo alisema kuwa pingamizi hilo huwa linadumu siku 30 na mweka pingamizi huwa anapewa muda huo kuwasilisha amri ya mahakama na asipofanya hivyo zuio hilo linakuwa limeondolewa.
Pia alisema kuwa maombi ya mabadiliko ya umiliki yanapowasilishwa husubiri mpaka siku 30 ili kuona kama hakutakuwa na pingamizi ndipo hufanyika mabadiliko.
Hata hivyo, Apollo hakuwa tayari kueleza ni lini mabadiliko hayo yalifanyika akidai kuwa si msemaji wa hilo isipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Katibu Mkuu alipotafutwa hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi (sms).
Hata baada ya kuandikiwa barua na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali aliposhauri pia atumiwe barua hiyo aifikishe mahali husika na akakiri kuiwasilisha mahali husika, lakini mpaka leo ni zaidi ya mwezi mmoja na nusu haijajibiwa.
Hata hivyo, licha ya Apollo kueleza kuwa mabadiliko ya umiliki hufanyika baada ya siku 30 tangu kupokea maombi, na licha ya kukataa kueleza ni lini mabadiliko ya umiliki wa nyumba hiyo yalifanyika kumbukumbu za Mahakama zinaonesha kuwa mabadiliko hayo yalifanyika siku mbili tu baada ya Matimbwa kuwasilisha maombi hayo.
Pia licha ya Mwananchi kuwasilisha maombi ya upekuzi kujiridhisha na ukweli hali ya umiliki wa nyumba hiyo kwenye mfumo na licha ya kulipia gharama zote na Apollo akaahidi kutoa taarifa hiyo siku iliyofuata, mpaka leo takribani miezi miwili hajatoa taarifa hiyo.
Vilevile licha ya Apollo kudai kuwa taarifa za mabadiliko ya umiliki wa nyumba hiyo zingefanyiwa marekebisho kwenye mfumo siku iliyofuata baada ya mabadiliko hayo kufanyika kwenye jalada, hata hivyo mpaka leo hakuna mabadiliko yoyote.
Hata hivyo, ankara ya malipo ya kodi ya ardhi ya Julai 9, 2026 inaonesha kuwa bado umiliki wa nyumba hiyo haujawahi kubadilishwa kwani bado uko katika jina la Abrahamsson.