
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa mazungumzo yaliyofanyika kati ya Iran na Marekani yalianzishwa kwa kuzingatia misingi ya heshima, maslahi ya taifa, busara na hadhi ya Iran.
Pezeshkian amesisitiza kuwa, licha ya kuendelea mazungumzo hayo, diplomasia ya Iran haitawahi kulegeza msimamo wake katika kutetea haki halali za wananchi na taifa la Iran. Aliongeza kuwa serikali itaendelea kusimamia kwa uthabiti maslahi ya taifa na haitakubali shinikizo lolote litakaloifanya iachane na haki zake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesema maadui waliianzishia Iran vita vya pande zote kwa lengo la kuibua shinikizo la ndani na kusababisha kusambaratika kwa mshikamano wa kijamii, lakini walishindwa kufikia malengo yao.
Pezeshkian amesema wazalishaji na wenye viwanda wa Iran walionyesha ustahimilivu wa kipekee kwa kuendelea na shughuli za uzalishaji licha ya changamoto mbalimbali, jambo lililozifanya dola kubwa kushindwa kutekeleza mipango yao.
Rais wa Iran ameongeza kuwa kushindwa huko kulizilazimu nchi hizo kubadili mkakati wao na kuelekea kwenye njia ya mazungumzo na maingiliano badala ya kuendelea na mwelekeo wa vita.
Dkt. Masoud Pezeshkian, amesema mafanikio ambayo Iran imeyapata yametokana kwa kiasi kikubwa na miongozo na uungaji mkono wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa serikali na sekta ya uzalishaji.
Pezeshkian amesema anaamini kwa dhati kwamba kila mafanikio yaliyopatikana ni baraka ya maelekezo ya kiongozi huyo, ambaye daima alikuwa mstari wa mbele katika kuisaidia serikali. Aliongeza kuwa kila alipobaini dosari au mapungufu, alikuwa akishauri mamlaka husika kwa upole na faraghani.
Rais Perzeshkian amesisitiza kuwa hata sasa, Iran ingali inahitaji uungaji mkono wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kwamba serikali itaendelea kusonga mbele kwa nguvu na azma katika kutekeleza majukumu yake.