Dar es Salaam. Toka enzi walipoanza kutamba kwenye ulimwengu wa filamu za Kibongo, wameendelea kubaki kwenye rada za mashabiki kwa kila hatua wanayopiga, mbali na kazi za uigizaji zilizowajengea majina katika jamii, wameanzisha jukwaa jipya la maudhui linaloendelea kuwafanya wazungumzwe kila siku.

Je, unajua ni nani hao: Ni kundi la A-List linaloundwa na warembo wakali Kajala Masanja, Irene Uwoya, Aunty Ezekiel na Jacqueline Wolper, ambao kwa sasa wanatikisa mitandao mbalimbali ya kijamii kutokana na uwezo ambao wameendelea kuuonyesha huko.

Walianza kwa kushirikiana kutengeneza maudhui kupitia YouTube na sasa wamepanua wigo kwa kuwa na kipindi kinachorushwa kwenye televisheni, hatua inayozidi kuongeza ushawishi wao kwa jamii, kuendelea kuwafuatilia kila wanachokifanya.

Moja ya vitu ambavyo wanavifanya A List ni kuzungumzia maisha yao halisi (Exclusive), na kufafanua vitu ambavyo vimewahi kusikika kama tetesi kwenye jamii, jambo lililopokelewa kwa kishindo na mashabiki wao, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

WANAWASHANGAZA GEN Z

Walijizolea umaarufu miaka mingi iliyopita, mastaa hao wameonyesha uwezo mkubwa wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia, kile kilichotarajiwa kufanywa na Gen Z wanakifanya na bado majina yao yanatajwa kila kona kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakiuvaa uhusika vizuri.

KUTUNZA UREMBO

Moja ya silaha kubwa wanazotumia ni kulinda muonekano wao, hawapitwi na fasheni za mavazi na kugeuka mfano wa kuigwa kwa wanawake wengi kupenda aina ya uvaaji wao, mfano mzuri ni namna Kajala ambavyo anafanya mazoezi ya gym ambayo yanamfanya awe na shepu ya kuvutia na kila siku amekuwa akionekana kijana.

MAHUSIANO YAO

Maisha yao ya kimapenzi yamekuwa yakivuta hisia za watu kwa muda mrefu, wakati mwingine kupitia taarifa wanazoweka wenyewe, nyingine zikiwa ni tetesi, mahusiano yao yameendelea kuwafanya wabaki kwenye vichwa vya habari na kuzua mijadala kwa mashabiki.

Mfano mojawapo ni Kajala na Harmonize wamekuwa wakiachana na kurudiana, jambo ambalo likizungumzwa zaidi na mashabiki kutokana na umaarufu wa wawili hao pia utofauti wa umri.

Kwa Aunty Azikiel miongoni mwa mahusiano yake yaliyokuwa yanazungumzwa zaidi na mashabiki yao ilikuwa mzazi mwenzake Mose Iyobo, ukiachana na huyo kuhusu mwanamuziki Kusah aliyezaa naye watoto wawili katika kipindi chao aliwahi kukiri alifunga ndoa ya kimyakimya na msanii huyo wa Bongo Fleva.

Kwa Uwoya ambaye kwa sasa kuna tetesi za kutoka kimapenzi na msanii Mboso pia mume wake marehemu Hamad Ndikumana aliyewahi kuichezea Simba na Stand United, ukiachana na huyo aliwahi kuhusishwa kuwepo kwenye mapenzi na msanii wa Bongo Fleva Dogo Janja, ingawa hilo alilipinga kwenye kipindi chao na alisisitiza aliwahi kuwa na ndoa moja tu, huku Aunty Azekiel akibakia anamshangaa na kumhoji walichokiona ilikuwa ni muvi au ndoa.

Kwa upande wa Wolper kabla ya kuachana na msanii wa Bongo Fleva Hamonize ambao ulikuwa kati ya uhusiano ulikuwa unazungumzwa zaidi mitandaoni, ila kwa sasa ana ndoa yake na Rich Mitindo.

KUZUNGUMZIA MAISHA YAO

Tofauti na mastaa wengi wanaoficha maisha yao binafsi, wao hawasiti kushirikisha jamii mambo yao, mfano mzuri ni namna ambavyo wanaelezea walivyokuwa wanahongwa pesa nyingi kipindi walipoanza kuwa maarufu na mikasa tofauti ya kimahusiano na maisha.

Exclusive zao zinazozidi kuwasogeza kwa jamii ya Gen z wengi waliyokuwa wanawaona kwenye muvi na sasa wanapata muda wa kusikiliza kile ambacho hawakuwahi kukisikia.

Uwoya aliwahi kuwashangaza wenzake baada ya kusimulia stori ya aliwahi kufungwa nchini Zambia:”Niliwahi kukaa jela miaka miwili, nilikamatwa na paspoti za kusafiria kama 25 za kwangu ambazo zilikuwa na sura yangu, nilikutana na mwanaume Uganda ambako nilikuwa nasoma, kipindi hicho nilikuwa na paspoti ya karatasi.

Anaongeza:”Huko ndiko nilikokutana na huyo mwanaume akaniita malaika, sikumuitikia akaja kwa mbele yangu na kunipa mkono, baada ya hapo sikurudi nyumbani hadi nilipokwenda kukamatwa Zambia na mama mzazi ndiye aliyekuja kunitoa”.

KUJIPA THAMANI MBELE YA JAMII

Pia wamejijengea utamaduni wa kuchagua mazingira wanayoonekana, ni nadra kuwaona katika sehemu zinazoweza kuharibu taswira zao, mara nyingi huonekana kwenye shughuli rasmi na za kijamii kama harusi, misiba, sherehe za kuzaliwa, uzinduzi wa bidhaa, kampeni mbalimbali na matukio ya kijamii, hali inayochangia kulinda hadhi za kuonekana wapya kila wanapoonekana mbele ya hadhara ya watu.

WAJASIRIAMALI

Pamoja na umaarufu wao, wanaonekana kujishughulisha na ujasiriamali, jambo linalowafanya wajitegemee kipato na kuendelea kuishi maisha ya juu.

Kutokana na wanachokifanya, msanii Harmonize aliwahi kuzungumzia kwamba:”Wanachokifanya wanapaswa kujifunza mabinti wengi, hadi vipindi vyao vimepata nafasi kwenye tv ina maana ni watu ambao wanafuatiliwa na wengi.”

Mwingine aliyelizungumzia hilo ni msanii wa muziki, Nedy Music aliyesema:”Ni wanawake ambao wamefanya mambo makubwa kwenye kiwanda cha Bongo Muvi na bado wamekuja na kitu kipya ambacho kitawaingizia kipato, wanaonyesha ni wabunifu wa kuitumia vizuri mitandao.”

Awali A List ilikuwa na wasanii wengine kama Wema Sepetu na Elizabeth Michael ‘Lulu’ ingawa kwa sasa hawaonekani sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *