WIZARA ya Afya Zanzibar, imeipongeza timu ya netiboli ya Afya Sports Club Zanzibar kwa kuondoka na tuzo tatu katika mashindano yaliyofanyika Dodoma ambapo imeshika nafasi ya tatu, pia ikitangazwa kuwa timu yenye nidhamu na kuambulia tuzo ya mchezaji bora.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Mngereza Mzee Miraji katika hafla maalumu ya kuipokea na kuipongeza timu hiyo baada ya kurejea kutoka kwenye mashindano hayo.

Akizungumza katika hafla hiyo, kiongozi huyo amesema mafanikio yaliyopatikana yanaonesha dhamira, nidhamu na mshikamano wa wachezaji pamoja na viongozi wa timu hadi kufikia hilo.

Amesema ushindi huo ni mafanikio makubwa yanayothibitisha michezo imeendelea kuwa sehemu ya kuitangaza wizara na kuimarisha ushikamano wa watumishi.

“Matarajio ya wizara ni kuona timu hii ikiendelea kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji Wizara hiyo, Rashid Hamdu Makame, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya maandalizi mazuri, nidhamu na kujituma kwa wachezaji pamoja na viongozi wa timu.

Aliwahimiza wanamichezo kuendelea kudumisha nidhamu, mshikamano na kujituma ili kuendelea kuiletea heshima wizara katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Naye Katibu wa timu hiyo, Mohamed Mihambo, amesema walishiriki mashindano hayo yaliyozikutanisha timu nane kutoka taasisi mbalimbali nchini, ambapo ilicheza mechi saba, imeshinda nne, sare moja na kupoteza mbili, hivyo  kumaliza nafasi ya tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *