YANGA imemtambulisha winga Erick Mwijage ambaye amesajiliwa akitokea KMC iliyoshuka daraja, sasa jamaa wameibuka wakisema mabingwa hao wamekosea kumsainisha mchezaji mwenye mkataba na klabu nyingine.
Mwijage amesaini mkataba wa miaka miwili akitua Yanga na juzi usiku akatambulishwa rasmi na mabingwa hao kuwa mchezaji wao mpya kwa msimu ujao.
Kama hujamzingatia, Mwijage ni winga mwenye akili nyingi uwanjani akijua kufunga na hata kupenya kwenye ukuta wa wapinzani akiwahi kuzitumikia Geita Gold na Kagera Sugar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Samson Madenyeka, amesema wameshangaa kuona Yanga ikifanya makosa ya kumsainisha mchezaji ambaye bado wana mkataba naye.
Madenyeka amesema Yanga wameonyesha kuwadharau kwa hatua waliyofanya na kwamba hata kama klabu yao imeshuka daraja haifanyi mikataba kutotambulika.
“Tumeshangaa sana kuona Yanga klabu kubwa inafanya mambo kama haya, Mwijage ni mchezaji wetu na alisaini mkataba wa miaka miwili, ameshatumikia mwaka mmoja na amebakiza mwaka mmoja,” amesema Madenyeka.
“Kwanza tuliona wanaomba tumuidhinishe (Mwijage) kwenye mfumo wa usajili, sisi tuligoma, kiongozi wao mmoja akatupigia tukamwambia, hatutamuidhinisha Mwijage kwa kuwa bado ana mkataba kwetu.
“Unajua kinachotusikitisha, Yanga ni klabu ambayo tunazungumza nao vizuri, hawakuwa na shida ya kuja kwetu na kuwapa taarifa kamili ya mkataba wa mchezaji lakini ni kama wameamua kufanya yaleyale ambayo waliyakosea huko nyuma.”
Aidha Madenyeka ameongeza kuwa, watafuata sheria zote kudai haki yao kwa hatua ambayo Yanga imefanya kwa kumtambulisha mchezaji mwenye mkataba na klabu nyingine.
“Hatugombani, KMC itafuata utaratibu wa kisheria tu kudai haki yake, unajua mpaka sasa wameshamtambulisha na kumvalisha sare za klabu, hili ni kosa kubwa, tutapita njia sahihi kudai haki yetu.”
Matukio kama haya yamekuwa yakijiri mara kwa mara katika usajili hapa nchini. Mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025, KMC ilikuwa na mvutano na Simba juu ya uhamisho wa kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu.
KMC ilimuwekea pingamizi Awesu kucheza Simba kwa madai kuwa hakufuata taratibu za kuvunja mkataba jambo ambalo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ikatoa taarifa kuwa Awesu ni Mchezaji halali wa KMC na kuvunja kwake Mkataba hakufuata taratibu. Baadaye yakafanyika makubaliano baina ya klabu hizo mbili na mchezaji, Awesu akaidhinishwa kuwa mchezaji wa Simba.
Hata hivyo, Yanga imesisitiza kwamba, ilifuata taratibu zote za usajili ndiyo maana ikamtambulisha winga huyo.