KAHAMA: Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Rose Manumba, amesema halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya Sh bilioni 9 katika mwaka wa fedha uliopita, sawa na asilimia 106 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 8.5.
Akizungumza katika kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Msalala, Manumba alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wa Serikali katika miundombinu, akimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora yanayowezesha ukusanyaji wa mapato. Pia alisema halmashauri tayari imepeleka asilimia 93 ya fedha zilizotengwa kwenye miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Mibako Mabubu, alisema ushirikiano kati ya watendaji wakiongozwa na Mkurugenzi pamoja na madiwani umechangia mafanikio hayo, akisisitiza kuwa wote wana lengo moja la kuijenga Msalala.
Alisema Msalala ni miongoni mwa halmashauri zinazofanya vizuri katika Mkoa wa Shinyanga, akieleza kuwa imefanikiwa kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara kwa kutumia mapato ya ndani.
“Niuambie umma kwamba Msalala inayozungumzwa vibaya siyo hali halisi. Sisi watendaji na madiwani tuna wimbo mmoja wa kuijenga Msalala, na atakayetubeza atakuwa na sababu zake binafsi,” alisema Mabubu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Six Ibrahim, alimpongeza Mkurugenzi Manumba kwa utendaji wake, akisema mafanikio yanayoonekana yanatokana na usimamizi mzuri wa shughuli za halmashauri.
Alisema bado wana imani na uongozi wa Manumba na kuomba aendelee kupewa nafasi ya kuisimamia halmashauri hiyo ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ikinda, Matilda Msoma, alimpongeza mkurugenzi huyo kwa kasi ya utendaji wake, akisema halmashauri imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuyatunza na kuyaelekeza kwenye vipaumbele vilivyopangwa.
Msoma alisema matumizi sahihi ya fedha yamewezesha miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa ufanisi na halmashauri kufikia malengo yake ya mwaka wa fedha.
