Watatu wafariki dunia kwa kujinyonga KilimanjaroWatatu wafariki dunia kwa kujinyonga Kilimanjaro

KILIMANJARO; WATU watatu, akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kotela Mashariki, wamefariki dunia kwa madai ya kujinyonga katika matukio tofauti yaliyotokea Julai 21 na 22, 2026 katika Kata za Mamba Kaskazini na Kilema Kati, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha matukio hayo na kusema mmoja wa marehemu Lameck Matowo (55), ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kotela Mashariki, aliyedaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwenye shamba la migomba Julai 21 majira ya saa 6 mchana,huku uchunguzi wa awali ukibaini chanzo cha tukio ni changamoto ya afya ya akili.

Mwingine ni Frank Gasper Makundi (54), fundi ujenzi na mkazi wa Komakundi, Kata ya Mamba Kaskazini,aliyedaiwa kujinyonga katika shamba la migomba siku hiyo hiyo. Polisi wamesema uchunguzi wa awali unaonyesha alikuwa na msongo wa mawazo baada ya kufiwa na mtoto wake miezi miwili iliyopita.

Kamanda Maigwa amesema tukio la tatu linamhusu Junuary  William maarufu Husein Muiraq (30), dereva bodaboda na mkazi wa Kimaroroni, Kata ya Kilema Kati, ambaye alidaiwa kujinyonga kwa kutumia shuka ndani ya chumba chake Julai 22 na kwamba  chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.

Diwani wa Kata ya Mamba Kaskazini, Leonard Ngowi, amesema vifo viwili vilivyotokea ndani ya siku moja katika kata hiyo vimewaacha viongozi na wananchi katika mshtuko mkubwa.

Kwa upande wake, ndugu wa marehemu Lameck Matowo, Felix Matowo, amesema familia haikuwahi kubaini dalili zozote za changamoto kwa marehemu, akieleza kuwa aliamka na kufanya shughuli zake kama kawaida kabla ya kukutwa amefariki shambani.

“Aliamka kama kawaida, akafanya shughuli zake za kulisha mifugo na kunywa chai kabla ya kuonekana akijitenga.Baadaye mama alipokuwa anamtafuta kwa ajili ya kumuuliza jambo fulani hakumuona, ndipo akamwomba jirani amsaidie kumtafuta.

“Walipoanza kumtafuta walimkuta shambani akiwa amejitundika juu ya mti. Hakuwa na tatizo lolote na mtu, alikuwa anaishi vizuri na jamii. Hadi sasa bado hatujajua ni changamoto gani iliyomsibu na kusababisha afikie uamuzi huo,” amesema Matowo.-

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *