Simiyu. Wakulima wa zao la pamba katika Jimbo la Maswa Mashariki, mkoani Simiyu wameiomba Serikali kufanya mapitio ya mfumo wa ununuzi wa pamba kwa kuruhusu wanunuzi wengi kushindana katika soko.
Wanasema hatua hiyo itaongeza ushindani wa bei, kuboresha kipato chao na kuhamasisha uzalishaji.
Wakizungumza leo Ijumaa, Julai 24, 2026 mbele ya Mbunge wa Maswa Mashariki, Dk George Lugomela, wakulima hao wamesema mfumo wa sasa wa mnunuzi mmoja katika eneo husika unawanyima fursa ya kuuza pamba yao kwa bei yenye ushindani.
Wamesema iwapo soko litafunguliwa na wanunuzi wengi kuruhusiwa kununua pamba, kampuni zitalazimika kushindana kwa bei na huduma, hali itakayomnufaisha mkulima na kuongeza thamani ya zao hilo.
Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki,Dkt George Lugomela akizungumza na wakulima wa zao la pamba katika Kata ya Busilili. Picha na Samwel Mwanga
Mkulima wa Kata ya Busilili, Jimola Jinunu amesema mfumo wa sasa umepunguza faida ya zao la pamba licha ya gharama kubwa wanazotumia kuandaa mashamba, kununua pembejeo na kuvuna.
“Tunaiomba Serikali itufungulie soko. Tukiwa na wanunuzi wengi kila mmoja atalazimika kutoa bei nzuri ili apate pamba yetu. Hapo ndipo mkulima ataanza kuona thamani ya jasho lake,“ amesema.
Naye mkulima wa Kata ya Bugarama, John Ngusa amesema mfumo wa mnunuzi mmoja unawalazimu wakubali bei wanazopewa kwa kuwa hawana mbadala wa kuuza mazao yao.
“Tunapolima tuna matumaini ya kupata faida, lakini tunapofika kuuza hatuna nafasi ya kujadiliana bei. Ushindani wa wanunuzi utasaidia kila kampuni kuboresha bei na huduma kwa wakulima,” amesema.
Kwa upande wake, mkulima wa Kata ya Nguliguli, Maiko Masanja amesema soko huria litawahamasisha vijana wengi kuingia katika kilimo cha pamba kutokana na uwezekano wa kupata bei nzuri.
“Kama kutakuwa na bei nzuri, vijana wengi watarudi mashambani. Kilimo cha pamba kinaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira na kipato endapo mkulima atalindwa na mfumo mzuri wa soko,“ amesema.
Naye Jimoga Shija wa Kata ya Senani amesema pamoja na wakulima kuendelea kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo, mafanikio yao yataongezeka zaidi iwapo Serikali itaruhusu ushindani wa wanunuzi badala ya mfumo wa mnunuzi mmoja.
“Mkulima akijua kuna wanunuzi wengi watakaoshindana, ataongeza uzalishaji na kuhakikisha analima kwa ubora. Ushindani huo utanufaisha mkulima, kampuni na Serikali kupitia ongezeko la uzalishaji,“ amesema.
Akizungumza na wakulima hao, Mbunge Lugomela amesema pamoja na umuhimu wa kuwa na soko lenye ushindani, wakulima wanapaswa kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba ili kuongeza thamani ya zao hilo.
“Umefika wakati wa kuzalisha pamba kwa tija kwa kila hekari. Kadri uzalishaji na ubora unavyoongezeka, ndivyo thamani ya zao hilo katika soko inavyoongezeka na mkulima anapata manufaa zaidi,” amesema.
Sehemu ya wananchi wa Kata ya Nghigwa waliojitokeza kwenye mkutano wa wakulima na Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki Dk George Lugomela. Picha na Samwel Mwanga
Amesema Serikali imeanzisha mfumo wa kutumia wataalamu wa mpango wa Building Better Tomorrow (BBT) kuwasaidia wakulima kupata elimu ya kilimo bora cha pamba, matumizi sahihi ya pembejeo na usimamizi wa mashamba ili kuongeza uzalishaji.
Amefafanua kuwa kampuni za ununuzi wa pamba hugharamia wataalamu hao kwa makubaliano ya kununua pamba katika maeneo wanayoyahudumia.
“Wataalamu hao huwapatia wakulima pembejeo na elimu ya kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba ili kuongeza tija na ubora wa zao,“ amesema.