
Dar es Salaam. Katika enzi hii ya teknolojia na mabadiliko ya maisha ya kila siku, imekuwa ni nadra kuwaona watoto wakikusanyika na kucheza kwa pamoja mitaani.
Awali ilizoeleka inapofika jioni baada ya watoto kurudi shule au kipindi cha likizo, watoto katika mtaa husika hukusanyika na kufurahi pamoja kwa kucheza michezo mbalimbali.
Baadhi ya michezo hiyo ni pamoja na mpira wa miguu, kombolela, rede, kula mbakishie baba, golori, bao, karata na ana nyingine za michezo ya kitoto.
Kwa miaka mingi michezo hiyo imekuwa sehemu ya watoto kukusanyika, kufurahi pamoja na kujifunza masuala mbalimbali.
Hata hivyo, kwa miaka ya hivi karibuni, utamaduni huo unaonekana kufifia katika baadhi ya maeneo.
Wataalamu wa afya na malezi wanasema mtoto kuchangamana na kucheza pamoja na watoto wenzake, ni jambo muhimu katika ukuaji wake.
Nini kinasababisha hilo
Akizungumza na Mwananchi, Amina Hassan ambaye ni mama wa watoto watatu anasema kwa upande wake anafikiri moja ya sababu ya utamaduni wa watoto kukusanyika pamoja na kucheza kufifia, ni mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
“Zamani tulikuwa tukiona watoto wakikusanyika na kucheza michezo mbalimbali ikiwemo kombolela, kuruka kamba au kuunda timu za mpira mtaani hasa nyakati za jioni. Siku hizi hiyo hali imekuwa ikipungua. Moja ya sababu ni mapinduzi ya teknolojia ambayo yamechangia uwepo wa simu janja na vifaa vingine vya kidigitali ambavyo watoto huvitumia kujifunza na kucheza michezo mbalimbali kupitia program zilizopo katika vifaa hivyo, ”anasema Amina.
Pia anasema sababu nyingine inaweza ikawa ni hofu tu ya mzazi juu ya usalama wa mtoto wake dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia au ajali hasa kama wanacheza karibu na barabara.
Kwa upande wake, Peter Paul ambaye ni baba wa mtoto mmoja anasema sababu nyingine zinazosababisha hilo ni zile za kimasomo pamoja na malezi ya usasa.
“Utamaduni wa maisha ya kisasa pia umeathiri, vilevile baadhi ya watoto wanapotoka shuleni huenda kusoma masomo ya ziada ‘twisheni’ wanaporudi nyumbani wakati mwingine huwa wamepewa ‘homework’ hivyo hujikuta wakikosa muda wa kucheza pamoja na wenzao mtaani,”anasema.
Wataalamu wa afya, malezi wanena
Ofisa mkunga msaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga anasema mtoto anapokosa fursa ya kuchangamana na wenzake mara kwa mara, inamnyima mtoto fursa ya kuchangamsha ubongo wake na kujifunza vitu vilivyopo katika mazingira.
Anaeleza kuwa kwa mtoto wa chini ya miaka miwili huweza kumuweka katika hatari ya kuchelewa kuzungumza katika ukuaji wake.
Anaongeza kuwa mtoto ambaye anapata fursa ya kucheza na watoto wenzake ni rahisi kujifunza lugha hivyo kama hana changamoto zingine ana nafasi kubwa ya kuwahi kuanza kuongea kuliko yule ambaye anafungiwa ndani.
“Kama mtoto mdogo hachezi na watoto wenzake, amefungiwa ndani tu hakuna wa kuongea naye mara kwa mara, muda wake mwingi anaangalia tu televisheni au kuchezea simu akiwa katika umri mdogo inaweza kumfanya kuchelewa kuongea”anasema.
Anasema mtoto anapocheza na wenzie huwa ni njia mojawapo ambayo huchangamsha mwili wake na hujifunza maneno mapya, huyabeba na kuyatumia kila siku.
Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Fredrick Mashili, anaeleza kuwa mtoto kuangalia televisheni au vifaa hivyo vya kidijitali kwa muda mrefu, kunaweza kumnyima fursa ya kuchangamana na watoto wenzake.
Anasema moja ya athari kubwa ni kupungua kwa shughuli za kimwili, Watoto wanapokuwa mbele ya televisheni kwa saa nyingi, wanapoteza muda wa kucheza au kufanya mazoezi ya mwili.
“Hii inaweza kuongeza hatari ya kupata matatizo kama vile uzito kupita kiasi ambalo ni tatizo linalozidi kuwa kubwa ulimwenguni, “anaeleza.