Uingereza imefuta zoezi kubwa la kijeshi nchini Kenya baada ya pande hizo mbili kushindwa kutatua mzozo kuhusu mamlaka ya Nairobi ya kuwafungulia mashtaka wanajeshi wa Uingereza wanaotuhumiwa kutenda uhalifu katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Zoezi lililopangwa la Haraka Storm, likihusisha Kikosi cha 1 na Kikosi cha The Duke of Lancaster’s Regiment, lilitarajiwa kuanza mwezi Septemba katika Kaunti ya Laikipia, katikati mwa Kenya. Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian lenye makao yake London, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema zoezi hilo sasa litafanyika nje ya Kenya.

Gazeti la Standard la Kenya limeripoti kuwa mafunzo hayo yamehamishiwa katika nchi jirani ya Tanzania.

Kenya ni ni mwenyeji wa kitengo cha kudumu cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza, kinachojulikana kama BATUK, katika mji wa Nanyuki, takriban kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu, Nairobi. Wanajeshi wa Uingereza wamekuwa wakifanya mafunzo hapo tangu Kenya ilipopata uhuru mwaka 1963, wakitekeleza mazoezi ya askari wa miguu, pamoja na shughuli za kihandisi chini ya makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo, wabunge wa Kenya wamezuia kuidhinishwa kwa upya kwa makubaliano ya  kijeshi baina ya nchi hizo mbili, huku wakitaka mamlaka makubwa zaidi ya kisheria juu ya makosa makubwa yanayotendwa na wanajeshi wa Uingereza.

Askari wa Uingereza walioko Kenya wanakabiliwa na tuhuma pana za utovu wa nidhamu, zikiwemo mauaji, ubakaji na uchafuzi wa mazingira. Ripoti ya uchunguzi wa miaka miwili ya bunge la Kenya iliyotolewa Desemba mwaka jana iliwashtumu wanajeshi wa Uingereza kwa mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na kuwafurusha kwa nguvu wakazi wanaoishi karibu na Nanyuki. Ripoti iliashiria jinai kama vile vifo na majeraha ya raia yaliyosababishwa na mabomu yasiyolipuka, uchafuzi wa mazingira, utupaji wa taka zenye sumu, pamoja na uharibifu wa makazi ya wanyamapori wakati wa mazoezi ya kijeshi na mafunzo.

Mwanajeshi wa zamani Robert Purkiss amefunguliwa mashitaka nchini Kenya kuhusiana na mauaji ya mwaka 2012 ya Agnes Wanjiru aliyekuwa na umri wa miaka 21. Hivi sasa anapinga kupelekzwa  Kenya kujibu mashtaka.

Mwaka jana, Uingereza ilikubali kulipa pauni milioni 2.9 sawa na dola milioni 3.9 kwa zaidi ya Wakenya 7,700 pamoja na kundi moja la mazingira kutokana na moto wa nyika wa mwaka 2021 uliowashwa na wanajeshi wa Uingereza wakiwa katika mazoezi. Moto huo uliharibu zaidi ya ekari 12,000 katika eneo la Lolldaiga Hills na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Kenya, Nelson Koech, amesema Nairobi inataka hatua madhubuti zaidi za uwajibikaji, ulinzi zaidi kwa jamii za wenyeji, pamoja na utekelezaji wa mapendekezo ya uchunguzi kuhusu askari wa Uingereza walioko nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *