
Dar es Salaam. Kuishi muda mrefu si suala la kuongeza idadi ya miaka pekee, bali ni kuhakikisha miaka hiyo inaambatana na afya njema, uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku.
Hilo ndilo linalozidi kuwa mjadala muhimu duniani, hasa wakati ongezeko la umri wa kuishi linavyoifanya jamii kuwa na idadi kubwa zaidi ya wazee.
Wataalamu wa afya wanasema lengo si kuishi miaka mingi ukiwa dhaifu na tegemezi, bali kuendelea kuwa na nguvu, uwezo wa kufikiri vizuri na kufanya shughuli zako kwa uhuru hata katika uzee.
Katika ripoti maalumu ya Pathways to Longevity iliyochapishwa na Harvard Health Publishing mwaka 2026, Daktari wa tiba ya maisha marefu (longevity medicine), Dk David Barzilai wa Marekani, ambaye pia ni mhadhiri wa Harvard Medical School, anataja mambo matano muhimu yanayoweza kuongeza nafasi ya mtu kuishi maisha marefu yenye afya.
Kwa mujibu wa Dk Barzilai, maendeleo ya tafiti za kisayansi yanaonyesha kuwa, pamoja na mchango wa vinasaba, mtindo wa maisha una nafasi kubwa katika kuamua ubora wa afya kadri mtu anavyozeeka.
Nchini Tanzania, takwimu za Serikali zilizotumika katika Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2024 zinaonyesha wastani wa umri wa kuishi umeongezeka hadi miaka 66.2 kutoka miaka 52.6 mwaka 2003.
Hali hiyo, anasema inaongeza umuhimu wa kuhakikisha miaka hiyo inaambatana na afya bora na uwezo wa kujitegemea.
“Afya bora haina siri za ajabu. Kinachohusika zaidi ni mambo ya msingi ambayo watu wengi tayari wanayajua, lakini mara nyingi hushindwa kuyafanya kwa uendelevu kwa miongo mingi,” anasema Dk Barzilai.
Mazoezi ya mwili
Dk Barzilai anasema mazoezi ni miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za kuishi maisha marefu yenye afya kwa kuwa huimarisha mifumo mbalimbali ya mwili kwa wakati mmoja.
Anasema mazoezi huboresha matumizi ya insulini mwilini, afya ya ubongo, uimara wa mifupa pamoja na uwezo wa moyo na mapafu kufanya kazi kwa ufanisi.
Anashauri watu kufanya angalau dakika 150 za mazoezi ya kiwango cha wastani au dakika 75 za mazoezi makali kila wiki, sambamba na mazoezi ya kuimarisha misuli angalau mara mbili kwa wiki.
Pia, anasisitiza umuhimu wa kupunguza muda wa kukaa bila kufanya shughuli kwa kusimama au kufanya kazi nyepesi mara kwa mara, akieleza kuwa hatua hiyo husaidia kudhibiti sukari na shinikizo la damu.
Lishe bora
Kuhusu lishe, Dk Barzilai anasema chakula kinaathiri moja kwa moja mazingira ambayo seli za mwili huishi kila siku.
Anashauri ulaji wa vyakula halisi, protini ya kutosha, mafuta yenye afya na vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi, huku akihimiza kupunguza matumizi ya wanga uliokobolewa unaoweza kuongeza sukari kwenye damu.
Anasema mahitaji ya protini huongezeka kadri mtu anavyozeeka kwa sababu husaidia kuhifadhi misuli na kuimarisha uwezo wa mwili kujirekebisha.
Usingizi wa kutosha
Dk Barzilai anasema usingizi ni sehemu muhimu ya afya kwa sababu ndiyo kipindi ambacho mwili hujirekebisha.
Kwa mujibu wake, usingizi husaidia kuondoa taka za kimetaboli kwenye ubongo, kuimarisha kumbukumbu na kurekebisha homoni zinazodhibiti hamu ya kula pamoja na msongo wa mawazo.
Anasema watu wazima wanashauriwa kulala kati ya saa saba na nane kila usiku, huku wakidumisha ratiba ileile ya kulala na kuamka.
Kudhibiti msongo wa mawazo
Anasema msongo wa mawazo wa muda mfupi unaweza kuwa na manufaa katika kukabiliana na changamoto, lakini unapodumu kwa muda mrefu unaweza kuathiri afya ya moyo, kinga ya mwili, usingizi na mfumo wa kimetaboli.
Kwa sababu hiyo, anashauri watu kudhibiti msongo kwa kufanya mazoezi, kupata usingizi wa kutosha, kutumia muda katika mazingira yenye mwanga wa asili na kujenga mahusiano mazuri na watu wanaowaamini.
Nguzo ya tano ambayo, kwa mujibu wa Dk Barzilai, mara nyingi hupuuzwa ni mahusiano ya kijamii.
Anasema ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa watu wenye mahusiano imara ya kifamilia na kijamii huwa na nafasi kubwa ya kuishi maisha marefu yenye afya, ingawa wengi huzingatia zaidi lishe na mazoezi kuliko mahusiano yao.
Anawashauri wanaojisikia wapweke kuanza kwa hatua ndogo, ikiwemo kuwasiliana mara kwa mara na watu wanaowaamini, kushiriki shughuli za kijamii au kujitolea katika shughuli zinazowakutanisha na wengine.
Akihitimisha, Dk Barzilai anasema badala ya kutafuta njia za miujiza za kuongeza umri wa kuishi, watu wanapaswa kubaini eneo walilo dhaifu zaidi katika mtindo wao wa maisha na kuanza kuliboresha, kwa kuwa mabadiliko madogo yanayodumu kwa muda mrefu ndiyo yanayoweza kuleta tofauti kubwa katika afya na ubora wa maisha wakati wa uzee.