
Iran imesema kuwa mazungumzo kati yake na Oman kuhusu safari salama za meli katika Lango Bahari la Hormuz yamepiga hatua nzuri, lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika katika suala la usafirishaji kupitia njia hiyo muhimu ya maji.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baqaei ameeleza kuwa duru kadhaa za mazungumzo zilifanyika mjini Tehran Ijumaa na Jumamosi kati ya Manaibu Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Oman.
“Pande mbili zimejadili kanuni za pamoja na taratibu za utendaji ili kuhakikisha usafiri salama wa meli katika Lango-Bahari la Hormuz, na zimetilia mkazo na kusisitiza suala la kuheshimiwa haki za mamlaka ya kitaifa ya nchi mbili hizi za mwambao huo,” amesema Baqaei.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, mazungumzo ya Iran na Oman yamekuwa na tija na yamepiga hatua muhimu.
Ujumbe wa Oman uliondoka Tehran Jumamosi ya jana na mazungumzo ya kiufundi na kisiasa kati ya Tehran na Muscat yataendelea.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna mabadiliko katika hali ya usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari huo.
Marekani imekiuka Mkataba wa Maelewano (MoU) wa tarehe 17 Juni kati yake na Iran uliosimamiwa na Pakistan kwa kujaribu kufanya mazoezi ya kijeshi ya majini yasiyoidhinishwa katika Lango-Bahari la Hormuz, jambo lililopelekea Jeshi la Wanamaji la Iran kuzizuia meli hizo ili kutekeleza makubaliano hayo.
Juzi Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi alisema kuwa Marekani ndio chanzo kikuu cha kukosekana utulivu na amani katika Lango Bahari la Hormuz na maeneo jirani kufuatia kukiuka majukumu yake na kuvuruga utekelezaji wa pande mbili wa Kipengele cha 5 cha Hati ya Makubaliano (MoU).