
Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa karibu miundombinu yote ya Marekani katika mji wa Erbil, kaskazini mwa Iraq imeharibiwa.
Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia amesema kuwa Iran imesababisha uharibifu mkubwa kwa kambi za jeshi la Marekani na kwamba sehemu kubwa ya kambi hizo haiwezi tena kufanya kazi, hasa huko Erbil nchini Iraq ambapo karibu miundombinu yote ya Marekani imeharibiwa. Msemaji wa Jeshi la Iran alieleza haya jana jioni kupitia kipindi cha televisheni ya taifa.
Ameongeza kuwa Iran iko tayari kuendeleza operesheni zake za kijeshi kwa namna hiyo hiyo iwapo vita vitaendelea, hadi pale Marekani itakapoelewa kuwa haiwezi kulazimisha matakwa yake kwa wananchi wa Iran kupitia mashambulizi ya kijeshi.
Brigedia Jenerali Akraminia amesisitiza kuwa Iran sasa inatumia ndege zisizo na rubani (droni) ambazo ni za kisasa zaidi kuliko Arash-2, ambazo zina nguvu kubwa zaidi ya uharibifu, usahihi wa hali ya juu wa kulenga shabaha na zenye kuruka masafa marefu zaidi.
Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ameeleza kuwa Iran imetambulisha zana mpya zilizoipa uwezo mkubwa, jambo ambalo limeifanya anga ya nchi kuwa hatari zaidi kwa adui ikilinganishwa na ile vita vya siku 40.
Ameongeza kuwa Rais wa Marekani Donald Trump amekiri kwamba alitoa kiasi kikubwa cha silaha kwa makundi ya waasi yenye makao yake huko Erbil ili kufanya operesheni za kigaidi dhidi ya Iran.
“Hivi sasa makundi hayo yamedhoofika pakubwa na hayana uwezo wa kutekeleza operesheni, na hali ya sasa si tu kwamba haiendani na utabiri wa Marekani, bali pia imeisababishia nchi hiyo wakati mgumu,” amesema msemaji wa Jeshi la Iran.