Dar es Salaam. Kauli ya Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi ya kuwataka Watanzania wapambane kupata Katiba mpya imeibua mjadala kuhusu nafasi ya Serikali, utashi wa kisiasa na mustakabali wa mchakato huo.

Wakati baadhi ya wadau wakiona kauli hiyo imefufua matumaini ya kuanza mjadala wa Katiba mpya, wengine wanahoji kwa nini wananchi waambiwe wapambane kupata jambo ambalo ni haki yao na mamlaka za dola zinaweza kulianzisha bila mapambano.

Mjadala huo umeibuka wakati suala la Katiba mpya likiwa miongoni mwa ajenda muhimu za muda mrefu zinazogusa mfumo wa utawala, uchaguzi, uwajibikaji wa viongozi na mgawanyo rasilimali na madaraka nchini.

Kauli ya Dk Nchimbi pia imeibua mjadala mpana kuhusu nani hasa anapaswa kubeba jukumu la kuanzisha mchakato huo na ikiwa mazingira ya sasa yanaweza kuharakisha utekelezaji wake.

Wachambuzi wa masuala ya sheria, siasa na utawala wanasema uzito wa kauli hiyo unatokana na ukweli kwamba imetolewa na kiongozi wa juu serikalini, ambaye pia amewahi kushiriki katika maamuzi makubwa ndani ya CCM kama mtendaji mkuu na Serikali.

Kauli ya Nchimbi

Akiwa katika Mkutano mkuu wa Watetezi wa Haki za Binadamu Julai 25, 2026, Dk Nchimbi alisema angepata nafasi ya kuambiwa awaambie Watanzania neno moja la mwisho, angesema, “pambaneni mpate Katiba Mpya. Pambaneni mpate Katiba ambayo ina makubaliano ya wadau wote.”

Alisisitiza wapambanie Katiba itakayoleta mwafaka katika Taifa, itakayoipeleka mbele nchi miaka 50 ijayo, ambayo kila Mtanzania atajisikia fahari kujitambulisha kuwa anatoka nchi yenye Katiba inayojali maisha ya mtu na inayoheshimu haki za raia wake.

“Ili uwe na hakika ya kupata Katiba mpya, moja ya mambo muhimu sana ni utashi wa kupata Katiba wa Rais aliyepo madarakani. Nataka niwaambie bila kuwadanganya, kwa mujibu wa Katiba yetu, Rais anapokaa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri, baraza la mawaziri haliamui linashauri,” amesema.

Amesema hata ajenda za Baraza la Mawaziri anayeamua ziingie au zitoke ni mkuu wa nchi, hivyo akisema hii haitaingia miaka 100 haitaingizwa.

Ameeleza ndiyo maana alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM, wakati wa mchakato wa kuandaa rasimu ya Ilani, walitumwa watu kwenda kufanya utafiti wa kujua Watanzania wanataka nini na majibu yakawa wanataka Katiba mpya.

“Wakaja kuniambia Watanzania wanataka Katiba mpya. Nikamwambia mwenyekiti wa ile kamati, sikilizeni jamani, jambo hili zuri lakini sasa hivi tayari tuna mgombea wa urais na tunatarajia atakuwa Rais ni vizuri atuhakikishie kwamba atalitekeleza hilo, tusiweke kitu ambacho hakitatekelezwa,” amesema.

Amesema alikwenda kumwona Rais Samia Suluhu Hassan na kumweleza kwamba kamati ya ilani imemweleza moja ya mambo makubwa imeyabaini ni kwamba Watanzania wanataka Katiba mpya.

Dk Nchimbi, amesema alimwambia Rais Samia kuwa, “nimekuja kukuuliza una utashi, unataka hili jambo liingie kwenye ilani ya CCM?”

Amesema Rais Samia alimjibu akisema hata Tume ya Haki Jinai aliyoiunda, katika moja ya mapendekezo yake ilibaini kuwa Watanzania wanataka Katiba mpya na aliahidi atatekeleza, hivyo hawezi kuiacha ahadi hiyo, iwekwe kwenye Ilani.

Kigogo CCM amjibu

Miongoni mwa watu wa awali kuzungumzia kauli ya Dk Nchimbi, ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Rajabu Maganya aliyesema Katiba mpya inaletwa na ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030 ambayo hata mwaka haujaisha tangu imeanza kutekelezwa.

“Asitokee mtu au chama cha siasa, kinahamasisha mtu au Watanzania eti waipiganie Katiba mpya. Katiba mpya inakuja, kwani nani aliyeizuia Katiba mpya, kwani nani anasema hakutakuwa na huu mchakato wa Katiba mpya?” amehoji.

Maganya ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, amesema viongozi na wanachama wa chama hicho wamepata kuilinda CCM, hivyo wasikubali kuwavuruga viongozi wenzao.

Aibua maswali mazito

Sambamba na mtazamo wa Maganya, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amesema kauli ya Dk Nchimbi imeibua maswali mazito kuhusu dhamira na mwelekeo wa mchakato wa Katiba mpya nchini.

Amesema ikiwa ni kweli Rais Samia anatambua umuhimu wa Katiba mpya na tayari suala hilo limo katika ilani ya CCM, bado inahitaji ufafanuzi kwa nini wananchi wanaambiwa waipambanie badala ya kuona hatua za moja kwa moja za utekelezaji.

“Kama Rais anaitaka Katiba mpya na Serikali inatambua umuhimu wake, ni kwa nini Watanzania waambiwe waipambanie? Wanapambana na nani na kwa sababu gani?” amehoji.

Askofu Bagonza amesema kauli ya Dk Nchimbi imefungua mjadala mwingine kuhusu nani mwenye mamlaka ya mwisho katika kuanzisha mchakato huo na kwa nini kauli ya mwisho isisikike moja kwa moja kutoka kwa Rais mwenyewe.

“Rais amewahi kuzungumzia Katiba mpya, lakini kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyokuwapo nchini kumekuwa na sintofahamu. Nadhani umefika wakati wa Rais mwenyewe kulizungumzia kwa uwazi zaidi kuliko kutegemea wasaidizi wake,” amesema.

Aidha, amesema ipo hoja inayohitaji kujibiwa kuhusu matumizi ya Katiba iliyopo wakati wananchi na makundi mbalimbali yakiendelea kudai mabadiliko ya mfumo wa kikatiba.

Kwa mtazamo wake, anaona mjadala wa Katiba mpya haupaswi kuonekana kuwa jukumu la Rais pekee, bali unapaswa kuhusisha taasisi zote muhimu za Taifa ikiwemo CCM, Bunge na wadau wengine wa kisiasa na kijamii.

“Je, kupata Katiba mpya kunategemea mtu mmoja kutaka au ni jukumu la taasisi za Taifa? Hili ni swali ambalo Watanzania wanahitaji kulipata majibu yake,” amesema.

Amesema pia kuna mjadala wa msingi kuhusu iwapo Taifa linapaswa kwanza kufikia mwafaka ndipo lipate Katiba mpya, au Katiba mpya ndiyo itakayokuwa chombo cha kujenga huo mwafaka.

“Huhitaji kuvaa miwani kuona kwamba kuna dalili za kutoridhika katika sehemu mbalimbali za jamii. Swali ni kama hali hiyo inaweza kutengeneza mazingira bora ya kupata Katiba inayokubalika na wote,” amehoji askofu huyo.

Amesema jambo la msingi kwa sasa ni kutafuta njia za kurejesha imani, kujenga maridhiano na kuandaa mazingira yatakayowezesha kupatikana Katiba bora na inayokubalika na wananchi wengi.

Kwa upande mwingine, amesema mchakato wa Katiba mpya unahitaji ushiriki wa Bunge, chombo ambacho hata hivyo amesema kinazua mjadala mwingine kuhusu kiwango cha imani ya wananchi kwake katika kipindi cha sasa.

Amesema matukio mbalimbali yanayojitokeza katika jamii yanaonyesha umuhimu wa kuharakisha juhudi za kujenga mshikamano wa kitaifa badala ya kuendelea kuahirisha mjadala wa Katiba mpya.

“Katiba mpya ilipaswa kupatikana zamani. Kadiri tunavyozidi kuchelewa, ndivyo maswali na matarajio ya wananchi yanavyoendelea kuongezeka,” amesema.

Anastahili pongezi

Kwa upande mwingine, kauli hiyo ya Dk Nchimbi imepongezwa na Mchambuzi wa Siasa, Profesa Baraka Mfinanga, kitendo cha kuzungumzia Katiba mpya hadharani akiwa kiongozi mwandamizi serikalini, kinastahili kupongezwa.

“Si kawaida kusikia kiongozi wa ngazi hiyo akizungumza kwa uwazi kuhusu Katiba mpya. Hiyo ni ishara kwamba hoja hiyo haijafa bali inaendelea kuishi ndani ya mfumo wa uongozi,” amesema.

Hata hivyo, amesema kauli hiyo inapaswa kufuatiwa na hatua na mikakati ya utekelezaji, kwa kuwa wananchi wanahitaji ratiba, maandalizi na maelezo ya mchakato badala ya kuendelea kusikia ahadi na matumaini.

Amesema Katiba mpya ni suala la kitaasisi, siyo la watu binafsi.

“Nguvu ya hoja ya Nchimbi itakuwa kubwa zaidi ikiwa itaambatana na hatua za kisera zinazoonyesha dhamira ya kuifikisha nchi kwenye Katiba inayokubalika.”

Mtazamo huo unafanana na wa Mchambuzi mwingine wa siasa, Said Majjid, anayesema kauli ya Dk Nchimbi imefungua mjadala muhimu kuhusu mahali ulipo uwezo wa kuanzisha mchakato wa Katiba mpya.

“Anaposema utashi wa Rais ni muhimu, amekuwa mkweli kuhusu namna uamuzi wa mambo makubwa ya kisiasa yanavyofanyika ndani ya mfumo wa utawala wa Tanzania,” amesema.

Amesema pamoja na ukweli huo, wajibu wa kupata Katiba mpya haupaswi kubaki kwa mtu mmoja, bali taasisi za kisiasa, Bunge na wadau wengine wanapaswa kuonyesha msimamo unaoonekana mbele ya wananchi.

“Katiba bora inajengwa kwa ushiriki mpana na uamuzi wa pamoja. Kauli ya Nchimbi iwe mwanzo wa hatua za vitendo zitakazorejesha imani kwamba mchakato huo unaweza kutekelezeka,” amesema.

Ameonyesha ujasiri

Mbali na maoni ya wachambuzi hao, kauli ya Dk Nchimbo imeibua mjadala mpana mitandaoni, ikiwemo kauli ya mwanaharakati Maria Sarungi kupitia ambaye amendika kuwa Dk Nchimbi ameonyesha uungwana na ujasiri kwa maneno yake kuliko wanachama wenzake wa CCM.

“Umetumia muda kuongelea Katiba mpya na kutaka tupambanie. Kwa maneno haya mazuri umefanya jambo jema na wapo wengi ambao wamepata matumaini,” ameandika Maria.

Lakini, ameongeza: “Maneno mazuri hayatoshi kwa hatua nchi iliyofika kwa kuwa yalishatolewa na wengi, hivyo kinachothaminiwa zaidi ni matendo.”

Hoja kama hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila: “Vinahitajika vitendo zaidi ya maneno ya kisiasa kuhusu masuala ya nchi, ukiwemo mchakato wa Katiba mpya.

“Bavicha tumesema huu ni wakati tunaohitaji vitendo dhidi ya maneno. Hatuhitaji kauli tamu za kutufurahisha,” ameandika.

Amesema inajenga wasiwasi kusikia Katiba itapatikana kabla ya 2029 na 2030 wakati hadi sasa hakuna bajeti ya mchakato huo, wala kalenda ya matukio haionyeshi hilo.

Amesisitiza ni muhimu uwekezaji ukafanywa kwenye kuhakikisha mazingira ya kupatikana Katiba mpya ya wananchi, badala ya maneno ya propaganda.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Itifaki, Mafunzo na Elimu kwa Umma wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Edward Kinabo, ameandika kauli ya Dk Nchimbi inaibua maswali kuhusu nafasi ya Serikali katika kuendeleza ajenda ya Katiba.

Kwa mtazamo wake, kauli hiyo inaonekana kuhamisha wajibu wa Serikali kwenda kwa wananchi.

Katiba Mpya hupatikana kupitia uamuzi na mchakato rasmi unaoongozwa na Serikali, huku wananchi wakishiriki kutoa maoni na kuamua kupitia kura ya maoni.

Aidha, kauli ya Dk Nchimbi, amesema inaweza kutafsiriwa kama ishara ya ukosefu wa utashi wa kisiasa. Serikali inayotambua umuhimu wa Katiba mpya haihitaji kusubiri shinikizo la wananchi ili kuanzisha mchakato wa kuipata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *