Mradi wa ujenzi wa Uwanja utakaotumika kwa Fainali za AFCON 2026 umefikia asilimia 88 na utakamilika rasmi mwezi ujao.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla amefichua hilo leo Jumapili, Julai 26, 2026 katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Nchimbi uwanjani hapo kujionea maendeleo ya mradi huo.
“Hii ni sehemu tu ya mradi mzima wa Uwanja wa AFCON ambao unagharimu Sh338 bilioni na huu ni uwanja wa mazoezi. Na uwanja wote kwa kazi ambazo zinaratibiwa hapa, wameshafika asilimia 88.
“Na huko tunakoenda utakuta tayari taa zimeshawekwa. Skrini zimewekwa. Uwanja huu utakuwa na uwezo wa kuweka watazamaji 32 elfu lakini viti ambavyo vimeshawekwa ni viti 26,000.
“Kwa maana ya kazi ya uwanja aliopewa mkandarasi kwa maana ya uwanja mkubwa na huu hapa, vyote kwa pamoja vinaenda kwa asilimia 88.
“Uwanja huu utakamilika mwishoni mwa mwezi wa nane. Kwa hiyo tutakuwa na mwaka mzima, uwanja ukiwa umekamilika. Kwa sasa tunakimbizana na barabara,” amesema Makalla.
Akizungumza baada ya maelezo hayo, Dk. Nchimbi amepongeza kasi ya ujenzi wa uwanja huo, huku akiagiza kukamilishwa kwa haraka, barabara zinazoelekea uwanjani hapo.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana na kuwashukuru uongozi wa Wizara ya Habari lakini pia vilevile uongozi wa mkoa, wakandarasi, mshauri wa mwelekezi kwa kazi kubwa ambayo imefanyika hapa.
“Wakati Marais wetu wa Tanzania, Kenya na Uganda walipokubaliana nchi zetu tatu ziwe wenyeji wa michuano ya AFCON mwakani waliahidi mambo ambayo watayatekeleza kuhakikisha jambo litafanikiwa na moja ya mambo ambayo Rais Samia aliahidi ni kujenga kwa viwanja vipya kikiwemo hiki cha hapa.
“Hiyo ndio ilipelekea tukakubaliwa kwa sababu uongozi wa CAF ulijua kwamba ahadi zile zimetolewa na watu wazito na kwa bahati nzuri wakati ule mimi nilikuwa Balozi wa Tanzania, Misri ambako ndiko kikao cha mwisho cha CAF kilifanyika kutoa uamuzi na ahadi ya Tanzania ambayo ilitoka kwa Rais Samia ilifanyika,” amesema Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi ameongeza, “kwa hiyo kwakweli kwamba Rais wetu anatoa ahadi za kimataifa na zinatekelezwa kwa kiwango hiki, ni jambo linatia moyo sana. Kwa hiyo kwa kweli nawapongeza kwa kazi nzuri ya kusimamia ahadi ya Rais lakini tunamshukuru mwenyewe kwa kusimamia kuona kwamba fedha zinapatikana na wakandarasi wenye uwezo wanapatikana lakini pia maelekezo ya Rais kuhakikisha jambo hili linasimamiwa vizuri.
“Nitoe wito tu kwa agizo alilotoa Rais kuhusu kukamilika kwa hizi barabara zinazokuja hapa. Ni muhimu agizo la Rais lifanyiwe kazi kwa nguvu sana kuhakikisha heshima ya nchi yetu lakini pia heshima ya Rais wetu.”