Jeshi la Sudan limetangaza kuendelea kusonga mbele katika jimbo la Kordofan Kaskazini, likisema kuwa limeudhibiti mji wa Barah pamoja na miji mingine kadhaa baada ya operesheni za kijeshi dhidi ya vikosi pinzani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mafanikio hayo ni sehemu ya operesheni zinazoendelea za kurejesha udhibiti wa maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na wapiganaji wa upande unaopingana na serikali.

Jeshi la Sudan limesema linaendelea na oparesheni zake katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha usalama na kurejesha mamlaka ya serikali katika maeneo yote ya nchi.

Kwa mujibu wa gazeti la Sudan Tribune, msemaji wa muungano wa kijeshi wa Jeshi la Sudan na washirika wake, Mutawakkil Ali Wakil, amethibitisha kuwa vikosi hivyo vimefanikiwa kuyadhibiti na kuyaimarisha kiusalama maeneo ya Al-Barakah, Umm Siyalah, Umm Jarafah, Jabra Al-Sheikh na Barah.

Naye gavana wa Jimbo la Darfur, Minni Arko Minnawi, amesema kupitia taarifa aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii kuwa ushindi huo hauashirii mwisho wa mapigano, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya operesheni za kijeshi dhidi ya waasi.

Minnawi aliongeza kuwa katika operesheni hiyo ya kijeshi, iliyofanywa kwa umakini mkubwa, jeshi na washirika wake waliwasababishia waasi hasara kubwa za watu na vifaa vya kijeshi.

Vita nchini Sudan, ambavyo sasa vinaingia mwaka wake wa nne, vimesababisha mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya binadamu duniani, huku visa vingi vya unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji mwingine zikiendelea kuwaathiri raia. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *