Moshi. Serikali imeitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuelekeza nguvu katika kuzalisha wataalamu wabunifu wa sekta ya utalii kupitia kampasi yake mpya inayotarajiwa kujengwa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Imesema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya utalii, kuongeza thamani ya huduma za kitalii na kuchochea ukuaji wa uchumi katika kanda ya kaskazini, sambamba na kufanikisha azma ya taifa ya kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.

Kauli hiyo imetolewa Januari 21, 2026 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, alipotembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kampasi hiyo ambayo itahudumia mikoa ya kanda ya kaskazini.

“Tunataka CBE ya kanda hii ijikite katika kuzalisha wataalamu watakaoongeza thamani ya sekta ya utalii, siyo kuwa waajiriwa pekee bali pia wawe wamiliki na wabunifu wa miradi na makampuni ya kitalii,” amesema Londo.

Ameongeza kuwa kupitia mwelekeo huo, kampasi hiyo itakuwa suluhisho la changamoto za kitaalamu na kimuundo zinazoikabili sekta ya utalii nchini.

“Katika masomo yao, wanafunzi wanapaswa kupata mafunzo ya biashara ya utalii, ujasiriamali, masoko ya utalii, usimamizi wa biashara za utalii na ukarimu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa CBE, Profesa Edda Tandi Lwoga, amesema kampasi ya Moshi itakuwa ya tano kwa chuo hicho na itasaidia kuongeza udahili wa wanafunzi.

Amesema kwa sasa CBE ina wanafunzi 24,657, huku kukamilika kwa kampasi hiyo mpya kukitarajiwa kuongeza zaidi ya wanafunzi 2,000.

Akizungumzia hatua ya utekelezaji, Profesa Lwoga amesema usanifu wa majengo matatu ya awali umeanza kwa gharama ya Sh174 milioni na unatarajiwa kukamilika Machi mwaka huu.

“Awamu ya kwanza ya ujenzi itahusisha madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,000, hoteli ya nyota tatu yenye uwezo wa kulaza wageni 52 kwa wakati mmoja pamoja na mabweni ya wanafunzi,” amesema.

Ameongeza kuwa kampasi hiyo pia itakuwa kituo cha umahiri katika biashara ya utalii na ukarimu, kikitoa mafunzo maalumu yanayolingana na fursa za kiuchumi za ukanda huo.

Kwa mujibu wa Profesa Lwoga, mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia una thamani ya Sh17.4 bilioni na ujenzi wake utaanza rasmi baada ya kukamilika kwa taratibu za kifedha.

“Ujenzi unatarajiwa kuanza baadaye mwaka huu wa 2026 baada ya usanifu kukamilika Machi Mosi, ambapo tenda ya ujenzi itatangazwa,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, ameishukuru CBE kwa kuchagua wilaya hiyo na kuomba mchakato wa utekelezaji uharakishwe ili wananchi waanze kunufaika mapema.

“Wananchi watanufaika kuanzia hatua ya ujenzi kupitia biashara ndogondogo za vyakula na huduma, na baadaye kupitia ajira na fursa nyingine zitakazotokana na uwepo wa kampasi hii,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *