Seoul, Korea Kusini. Kauli za hivi karibuni za viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Korea zimeibua taharuki na mjadala mpana kuhusu heshima ya uhuru wa dini, baada ya serikali kutuhumiwa kulenga wazi kundi maalum la kidini kabla ya kukamilika kwa uchunguzi rasmi.

Wadau wa masuala ya kisheria wanasema hatua hiyo inaweza kwenda kinyume na Katiba ya nchi hiyo, hususan Kifungu cha 20 kinacholinda uhuru wa dini na kusisitiza kutenganishwa kwa dini na dola.

Mjadala huo umechochewa na kauli ya Rais Lee Jae-myung aliyenukuliwa Januari 12 akisema madhara ya kijamii yanayodaiwa kusababishwa na “dini fulani” yamepuuzwa kwa muda mrefu na kusababisha uharibifu mkubwa. Kauli hiyo ilifuatiwa siku iliyofuata na agizo la Waziri Mkuu Kim Minseok la kuanzisha uchunguzi wa pamoja, akitumia pia maneno kama “uongo” na “uzushi,” jambo lililozua maswali kuhusu mchakato wa haki na usawa wa kisheria.

Wachambuzi wa sheria wanasema matamshi hayo yanaweza kuathiri uhuru wa vyombo vya uchunguzi na mahakama kwa kutoa taswira ya hitimisho kabla ya uchunguzi kuanza rasmi. Pia wanahoji iwapo ni sahihi kwa serikali isiyoegemea dini kutoa tafsiri au hukumu kuhusu mafundisho ya kidini.

Shincheonji Kanisa la Yesu, ambalo limetajwa katika mijadala hiyo, limeeleza wasiwasi wake likidai kuna kuingiliwa kwa upande mmoja kutoka kwa mamlaka za serikali. Kanisa hilo limesisitiza kuwa masuala ya imani hayawezi kuamuliwa kwa misingi ya shinikizo la kisiasa au maoni ya wengi.

Katika kujibu tuhuma hizo, kanisa hilo limependekeza kufanyika kwa uchunguzi wa hadharani wa mafundisho ya Biblia ili kutatua tofauti za kitheolojia, likisema liko tayari kurekebisha makosa yoyote yatakayothibitishwa kwa ushahidi wa wazi. Hata hivyo, linasema hadi sasa halijapata majibu rasmi kwa pendekezo hilo.

Shincheonji pia limeeleza mchango wake katika jamii, likitaja ushiriki wake katika huduma za kujitolea wakati wa majanga na kampeni za uchangiaji damu. Linasema pamoja na hayo, limeendelea kukumbwa na tuhuma bila kuwasilishwa ushahidi maalum wa kisheria wa madhara yanayodaiwa, huku likidai kesi kadhaa za awali zilimalizika bila hatia.

Kanisa hilo limeonya kuwa kulengwa kwa kundi moja la kidini kunaweza kuweka msingi wa ubaguzi dhidi ya makundi mengine siku zijazo. Limesisitiza umuhimu wa serikali kurejea katika misingi ya utawala wa sheria, usawa na ulinzi wa haki za kikatiba za raia wote bila kujali imani zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *