Dar es Salaam. Karibu Kila bendi kubwa siku hizi huwa inakuwa na kundi la wasanii ambao kazi yao ni kucheza muziki jukwaani. Jina maarufu la wasanii hawa lilikuwa ni ‘Stage Show’. 
Siku hizi huitwa Wacheza Show au Madansa na mara nyingine huitwa wanenguaji, japo jina hilo halipendwi sana na wenye taaluma yao.  

Mara ya kwanza mimi kuiona stage show jukwaani ilikuwa mwaka 1962 wakati Dorothy Masuka na kundi lake lilipopita Iringa na kufanya onyesho katika ukumbi wa Highland Cinema, nilikuwa mdogo sana lakini kilichobakia kichwani ni kumbukumbu ya wachezaji wake waliovaa vibwaya na Dorothy Masuka akiimba wimbo wa Patapata. 

Hivyo suala la kucheza shoo si jambo jipya japo limepitia katika mabadiliko mbalimbali.  Katika miaka ya 60, wacheza show hawakuwa na nafasi sana katika bendi za muziki wa rhumba.

Bendi zilikuwa zikifanya maonyesho yaliyokuwa na malengo ya kuwafanya wapenzi wa muziki wacheze. Bendi nyingi wakati huo zilikuwa na taratibu za kutoa taarifa ya wimbo ambao ungefuatia, jambo ambalo kwa sasa limebakia katika baadhi ya vikundi vya taarabu.

Katika utambulisho wa wimbo, bendi ilitangaza jina la wimbo na staili ambayo wimbo huo ungepigwa. Wimbo ulipoanza wapenzi wa muziki walisimama na kujitosa kucheza, kila mmoja akionyesha jinsi alivyoweza kuicheza vizuri staili iliyokuwa ikipigwa, hivyo basi bendi ikipiga wimbo wake kwa mtindo wa Rhumba, Chacha, Borelo au Charanga, wapenzi walisakata muziki kwa staili husika.

Bendi nyigine pia zilikuwa na taratibu zilizotoa hata maelekezo ya aina ya nguo za kuvaa. Unadhifu ulikuwa muhimu katika kumbi nyingine. 

Kwa waliokuwa waingiaji wa muziki katika kumbi kama ukumbi wa Bandari Grill wa New Africa, au  Simba Grill wa Kilimanjaro watakumbuka kulikuwa na mtu mlangoni aliyekuwa na tai nyingi, ukifika mlangoni na shati bila tai unaazimwa tai na baada ya kuivaa ndio unaruhusiwa kuingia ukumbini.

Mtu aliweza kukataliwa kuingia ukumbini kama kavaa kaptula, kandambili na hata raba.
Haya turudi kwa madansa, katika miaka ya sitini bendi za vijana ambazo hazikupiga muziki wa rhumba zilikuwa zikisindikizana na vikundi vya madansa waliokuwa wakajiita majina kama Makumba Show, Tammi Show na kadhalika.

Vikundi hivi vilikuwa vikijitegemea havikuwa chini ya bendi yoyote na mara nyingine vilikuwa vikifanya maonyesho yao bila bendi.

Kwa mfano kikundi cha Tammi show, kilikuwa kikiongozwa na Adam Kingui, msanii mwenye hadithi ndefu  sana katika sanaa. Ujio wa Luambo Luanzo Makiadi na bendi yake ya TP OK Jazz mwaka 1973, akiwa amesindikizana na kundi la madansa, uliamsha utamaduni wa kuwa na madansa katika bendi za rhumba. 

Utamaduni ambao umedumu mpaka leo.  Safari ya fani ya madansa haikuwa rahisi, mfano; mwanzoni mwa miaka ya themanini, Umoja wa Vijana Mkoa wa Dar es Salaam ulipiga marufuku stageshow. 

Katika tamko hilo  ambalo lilitolewa kwenye gazeti liliangaza pia kupiga marufuku majina ya sifa ya wasanii kama vile Power Savimbi aliyekuwa hodari wa kuonyesha michezo ya kuonyesha nguvu kama vile kuvuta magari kwa nywele zake.

Jina hilo lilipigwa marufuku kutokana na kuwa lilikuwa jina na mpinga serikali ya Angola miaka hiyo. Tamko lile  pia ndio lilipiga marufuku shule za nasari kuitwa shule za vidudu na ndipo jina shule za chekechea kupata umaarufu.

Ilikuwa ni katika tamko hilo ulipopigwa marufuku wimbo wa bendi ya Orchestra Mambo Bado ulioitwa Bomoa tutajenga Kesho, wimbo ambo hata mimi nilishiriki nikiwa mwanamuziki wa bendi hiyo. 

Lakini hakika marufuku ya ‘Stage Show’ haikudumu sana kwani bendi ziliendelea na utaratibu huo kwenye madansi yao. 

Kulikuwa na wacheza show ambao walikuja kupata umaarufu mkubwa sana kama vile akina Abdallah Pangapanga, Chileshi Ally, Nkulu Wabangoi, Frida, Flora Homa ya Jiji, Ajelike Wakubenga, Eliza Kimondo na wengine wengi.

Mmoja wa madansa wakongwe ni Tabu Mambosasa, ambaye kwa sasa ni mwanamuziki muimbaji, alianza kuonekana baada ya kushinda kwenye mashindano ya kucheza dansi watoto, yaliyokuwa yakiendeshwa na bendi ya Orchestra Makassy pale katika ukumbi wa Amana, Ilala, mwaka 1988. 

Akapata ujasiri wa kujiunga na kundi la wacheza show la International Africa Show iliyokuwa ikiongozwa na Kwempa Risasi, kisha akahama na kujiunga na kundi la Makutano Dancing Troupe moja ya makundi mengi yaliyokuwa yakijiita Dancing Troupe, kisha akahamia katika kundi la DDC Kibisa. 

Kaka yake ambaye alikuwa golikipa maarufu enzi hizo Athumani Mambosasa,  alikuwa mpenzi wa bendi ya MK Group hivyo akamshawishi kujiunga na kundi hilo. Ilipoanzishwa Washirika Tanzania Stars Tabu akawa mmoja ya waanzilishi wa kundi hilo maarufu. 
Baadaye akapitia MCA International Band na baadaye Bantu Group. Dansa mwingine maarufu ambaye kwa sasa amejikita katika muziki wa singeli ni Nasra Semhando, ambaye ni ndugu na wanamuziki marehemu, mpiga drum Abbu Semhando (Baba Diana) na mpiga bezi marehemu Bakari  Semhando (Disfa).

Nasra alianza kazi ya kucheza show mwaka 2000, na bendi yake ya kwanza ilikuwa Mwenge Jazz Band, safari yake katika kazi hiyo ikampitisha Vijana Jazz Band, Fax Jazz Band, Mviko, Double M Sound, Extra Bongo, Bambino Sound, Mchinga Sound, TOT na Akudo Sound, akiwa na wenzie wa enzi zake akina Halima White, Queen Happy, Diana Aston Villa, waliokuwa maarufu enzi zao.

Wacheza show wakongwe wanakubaliana kuwa  mambo mengi ni tofauti. Katika makundi hayo ya zamani malipo yalikuwa aidha posho baada ya kila onyesho au mshahara wa mwezi, siku hizi ni posho tu ambayo ukiangalia mara nyingine thamani yake ni ndogo kuliko waliyokuwa wakipata zamani.

Na badiliko kubwa ni muda wa kucheza show, wakati zamani show ilikuwa muda mfupi usiozidi nusu saa kila dansi, na muda uliobaki wakiachiwa wapenzi wa dansi waserebuke, siku hizi muda mwingi zaidi unatumika kwa madansa kucheza na wapenzi wa muziki  kulazimishwa kuwa waangaliaji tu. 

Bendi nyingine zilikwepa kuwa na wacheza show wasichana kuondoa matatizo ambayo yalikuwa yakizikumba bendi hizo kutokana na mahusiano ya kimapenzi kati ya wanabendi, matatizo ya wivu na ugomvi yakawa yanapunguza sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *