HOSPITALI ya Taifa Muhimbili – Mloganzila imehitimisha kambi maalum ya upasuaji wa kuondoa mawe kwenye figo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya laser ambapo tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo Septemba 2025, wagonjwa 18 wamenufaika na matibabu hayo.

Kambi hiyo iliyoendeshwa kwa siku tatu imelenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliyofanywa na Serikali katika sekta ya afya na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo MNH –Mloganzila Dk Hamis Isaka amesema upasuaji wa kuondoa mawe kwenye figo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya laser umefanywa na wataalam wa ndani, na hospitali imedhamiria kuhakikisha kuwa huduma hiyo inakua endelevu.

Kwa mujibu wa Dk Isaka, matumizi ya teknolojia ya laser yameleta mapinduzi makubwa katika matibabu ya kuondoa mawe kwenye figo kwani upasuaji huo wa kisasa humsaidia mgonjwa kupata maumivu kidogo, kutokuwa na kovu wala kukatwa, huku mgonjwa akikaa wodini kwa muda mfupi wa siku moja hadi mbili.

“Upasuaji huu wa kisasa hutumia kifaa maalum cha laser kinachovunja mawe kuwa vipande vidogo vinavyotolewa kwa urahisi bila kufungua tumbo, mgonjwa huruhusiwa kurejea nyumbani ndani ya muda mfupi,” amefafanua Dk Isaka

Ameongeza kuwa katika kliniki za Urolojia MNH-Mloganzila, takribani wagonjwa 20 wapya hugundulika kuwa na mawe kwenye figo kila mwezi na wanawake wanaongoza kuwa na changamoto hiyo.

Hivyo amewashauri wananchi wanaopata dalili kama maumivu makali ya mgongoni au ubavuni, maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na damu, kukojoa mara kwa mara au homa kufika hospitalini mapema ili kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu.

Aidha mmoja wa wanufaika na matibabu hayo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini na kuleta teknolojia za kisasa zinazowasaidia wananchi kupata matibabu bora kwa gharama nafuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *