
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, serikali na jumuiya ya kibinadamu, leo Jumatano, Januari 28, wamewasilisha mpango wa kukabiliana na hali ya kibinadamu mwaka 2026. Mahitaji yanayokadiriwa ni dola bilioni 1.4 kusaidia watu milioni 7.3 wanaolengwa, hasa mashariki mwa nchi. “Hali ni mbaya,” ameonya mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini humo, Bruno Lemarquis.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Kinshasa, Paulina Zidi
“Hali haijawahi kuwa mbaya sana hivi.” Kulingana na Bruno Lemarquis, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) nchini DRC, zaidi ya waathiriwa 200,000 wa ukatili wa kijinsia, zaidi ya Wakongo milioni 26 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, zaidi ya watoto milioni 4 wanaougua utapiamlo mkali, ongezeko mara mbili la visa vya kipindupindu, na ongezeko la 80% la visa vya Mpox vimerekodiwa. Kwa hayo, kuna watu milioni 5.3 waliokimbia makazi yao, 700,000 kati yao wamekimbia makazi yao katika wiki za hivi karibuni pekee.
Na mwelekeo unaongezeka, anasema Eve Bazaiba, Waziri wa Masuala ya Kijamii na Hatua za Kibinadamu, ambaye anasema kwamba nchi inaendelea kukabiliwa na mgogoro “mgumu, mrefu, na ambao haujawahi kutokea”. Kwa hivyo, mahitaji ni makubwa, na zaidi ya dola bilioni 1.4 zinahitajika kwa ajili ya mwitikio kibinadamu mnamo mwaka 2026. Huu ni wito wa kuwasaidia watu wapatao milioni 7.3, huku ikikadiriwa kuwa karibu watu milioni 15 watakuwa na uhitaji.
Hata hivyo, huu ni upungufu ikilinganishwa na mwaka 2025, ambapo mahitaji yalikadiriwa kuwa dola bilioni 2.5. Upungufu huu unaonyesha mabadiliko katika mkakati: “Tulitaka kuwa wa kweli zaidi,” anaelezea mwanachama wa jumuiya ya kibinadamu. Kwa kifupi, mahitaji hayajapungua, lakini lazima yapewe kipaumbele. “Kupewa kipaumbele kwa kiwango cha juu” ndilo neno linalotumika.
Chaguo ngumu
Kwa hivyo wadau katika masuala ya kibinadamu walipambanaje kutoka watu milioni 22 wanaohitaji mwaka wa 2025 hadi milioni 15 mwaka wa 2026? Kwa kuongeza, kwa mfano, kizingiti cha udhaifu. Sasa umakini unaelekezwa kwenye visa muhimu zaidi na katika maeneo ambayo yamekumbwa na msukosuko: migogoro, majanga, magonjwa ya mlipuko…
Hili pia ni kweli kwa sababu, kila mwaka, mwitikio wa kibinadamu nchini DRC haufadhiliwi kwa kiasi kikubwa. Mnamo mwaka2024, 54% ya mahitaji yalitimizwa, ikilinganishwa na 24% mwaka wa 2025. Na kwa kupungua kwa kasi kwa misaada ya Marekani, chaguzi ngumu zilibidi zifanywe, ameelezea Bruno Lemarquis.
Mbali na hayo, misaada ya kibinadamu haiwezi kuwa mwitikio pekee. Kuna njia kadhaa za kupunguza mahitaji: suluhisho za kisiasa, kushughulikia sababu kuu za migogoro, kuzuia migogoro, na utekelezaji wa suluhisho endelevu.