
Waziri wa Usalama wa Iran amesema kuwa taifa la Iran halitaruhusu umoja wa kitaifa wa nchi hii udhoofishwe akisisitiza kuwa umoja wa taifa la Iran ndiyo nguzo kuu ya kukabiliana na vitisho vya nje.
Akizungumza katika hafla jana Jumanne, Esmail Khatib amesema kuwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wanajua vyema kwamba taifa la Iran halitaruhusu umoja wa ardhi ya nchi hii kupatwa na madhara na kwamba madhali Iran ina umoja na mshikamano hakuna kitisho chochote kitakachoifanya Iran kushindwa.
Khatib ameashiria rekodi ndefu ya hatua za uhasama dhidi ya Iran na kusema: Ili kufahamu uhakika wa mambo inatosha kutupia jicho historia ya Iran; ardhi ambayo mara kwa mara imeshuhudia dhuluma dhidi ya watu wake kwa jina la uhuru, haki za binadamu n.k.
Waziri wa Usalama wa Iran amesema haya kufuatia matamshi ya vitisho ya Rais Donald Trump wa Marekani ambaye hivi karibuni alitishia kuchukua hatua mpya za kijeshi dhidi ya Iran kuhusiana na kile alichokitaja kuwa namna Jamhuri ya Kiislamu inavyoshughulikia maandamano ya wananchi kuhusu suala la kiuchumi.
Januari 8 na 9, makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na Marekani, Israel na washirika wao yalianzisha wimbi la mashambulizi ya silaha dhidi ya vituo vya polisi, kambi za kijeshi na maeneo mengine nyeti, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya raia, katika miji kadhaa nchini Iran.
Hata hivyo, majeshi ya Iran yalichukua hatua haraka na kwa ufanisi na kufanikiwa kuwatia mbaroni vinara wa ghasia na kuwanyang’anya silaha za moto, zikiwemo silaha zilizokuwa zikielekea katika mji mkuu Tehran.