Kamanda wa zamani wa mitambo ya ulinzi wa anga wa utawala wa kizayuni wa Israel ameielezea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni moja ya madola makuu duniani kwa upande wa masuala ya anga na ulimwengu wa makombora, na akasema, Tehran itailenga Tel Aviv iwapo kutakuwa na shambulio lolote litakalofanywa na Marekani dhidi yake.

Gazeti la Kizayuni la Ma’ariv limemnukuu Brigedia Jenerali Zvika Haimovich, kamanda wa zamani wa mitambo ya ulinzi wa anga ya Israel akithibitisha kuongezeka uwezo wa kijeshi wa Iran katika miezi ya karibuni na kueleza: “ukweli wa mambo umezidi kuwa tata mno, kwa sababu katika uga huu hatuko peke yetu. Kuna upande mwingine pia, na mimi kimsingi ningependekeza kwamba, haifai kuwadogosha maadui zetu, hususan katika ulimwengu wa makombora na anga za mbali. Katika ulimwengu huu, Wairani ni miongoni mwa madola mkuu.”

Akielezea jinsi Iran ilivyojikita katika uzalishaji wa makombora, Jenerali Haimovich amesema: “baada ya vita, wao waligundua kwamba kama kuna kitu athirifu na chenye ufanisi, basi kitakuwa ni makombora. Kwa hivyo walirudi kwenye uundaji wa makombora. Wana makombora yanayolenga shabaha kiusahihi.”

Kuhusu uwezo wa makombora wa Iran, Haimovich ameongezea kwa kusema: “kulikuwa na idadi kubwa ya makombora kabla ya vita na yako pia leo hii”.

Jenerali huyo wa zamani wa jeshi la utawala wa kizayuni ameendelea kueleza: “changamoto kuu ni kukabiliana na kiwango hiki kikubwa, kwa hivyo mimi nadhani tulichokiona mwezi Juni kwa upande wa kiwango kinaweza kurudiwa tena kwa kiwango sawa na kile”.

Haimovich amemalizia kwa kusema: “tumeuona uwezo wao; wao wana uwezo wa kumimina mvua ya makombora kutoka Haifa hadi B’ir Sheba kwa lengo la kulemaza kwa kiwango kikubwa maisha ya kila siku ya Waisraeli ”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *