
Jimbo la Jonglei lina wakazi takribani milioni mbili, wengi wao tayari wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Taarifa ya WFP iliyotolewa mjini Juba inakadiria kuwa karibu asilimia 60 ya wakazi wa jimbo hilo wanatarajiwa kukumbwa na viwango vya dharura vya njaa katika msimu ujao wa njaa, kipindi ambacho upungufu wa chakula hufikia kilele chake.
“Kuongezeka huku kwa operesheni za kijeshi kumekuja katika wakati mbaya zaidi,” amesema Adham Effendi, Kaimu Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini.
Ameongeza kuwa “Dirisha letu la kuwafikia walio hatarini zaidi linaendelea kufungwa kwa kasi. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa.”
Msimu wa njaa wakaribia huku misaada ikizidi kuzuiwa
WFP imeonya kuwa mapigano mapya yanaweza kulazimisha idadi kubwa ya familia kukimbia makazi yao kutafuta usalama na chakula, jambo linalozidisha hali ya kibinadamu ambayo tayari ni mbaya kuwa mbaya zaidi.
Shirika hilo limesisitiza umuhimu wa kuanza mapema mwezi Februari kuhifadhi chakula na vifaa vya misaada karibu na maeneo yaliyo hatarini zaidi, kabla ya mvua kubwa kati ya Aprili na Julai kukata njia kuu za barabara na kuyaweka maeneo mengi katika hali ya kutengwa.
Bila hatua za haraka, wanawake, wanaume na watoto katika maeneo ya mbali wako katika hatari ya kukosa msaada wakati mahitaji ya chakula yanaongezeka kwa kasi.
“Tunazihimiza pande zote kulinda raia na wahudumu wa misaada, na kuruhusu usafirishaji wa msaada muhimu wa kibinadamu,” amesema Effendi.
Shughuli za kibinadamu bado zimekwamishwa
Upatikanaji wa misaada ya kibinadamu unaendelea kuwa changamoto kubwa. WFP imesema kuwa Kikundi cha Usafirishaji cha Kibinadamu kinachoongozwa na WFP pamoja na Huduma ya Ndege za masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa UNHAS, bado hazijapewa idhini na mamlaka husika kuratibu misafara ya barabarani na safari za anga kwa niaba ya jumuiya ya misaada ya kibinadamu.
Ukosefu wa idhini hiyo unazuia mashirika ya misaada kuwafikia watu wanaohitaji msaada na unatishia kuyaacha makundi mazima ya jamii bila msaada wa kuokoa maisha.
“Ni muhimu sana tushughulikie mara moja vizuizi hivi,” amesema Effendi. “Kwa kupatikana kwa njia salama na zisizozuiwa, WFP ina timu na uwezo wa kuwafikia familia zilizo hatarini zaidi. Maisha ya mamia ya maelfu ya watu yako hatarini.”
Mamilioni wanahitaji msaada kote Sudan Kusini
Kote nchini Sudan Kusini mwaka 2026, WFP inalenga kuwafikia watu milioni 3.3 walio hatarini zaidi kupitia misaada ya chakula cha dharura, lishe, chakula cha shule, programu za kujenga mnepo na misaada ya fedha taslimu.
Hata hivyo, shirika hilo limeonya kuwa bila kupunguzwa kwa haraka kwa mapigano na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika Jimbo la Jonglei, uwezo wake wa kutoa msaada kwa kiwango kinachohitajika wakati wa msimu wa njaa utadhoofika kwa kiasi kikubwa.