
Kwa mujibu wa WHO zaidi ya watu bilioni 1 duniani wameathiriwa na magonjwa ya NTDs, huku idadi inayokaribiana nayo ikikumbwa na matatizo ya afya ya akili. Watu walioathiriwa na magonjwa ya kitropiki yanayosababisha ulemavu au mabadiliko ya mwonekano wa mwili kama vile leishmaniasis ya ngozi, ukoma, filariasis ya mfumo wa limfu, mycetoma na noma wako katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na unyanyapaa na ubaguzi.
Pia Who imeonya kwamba dhana potofu kuhusu maambukizi na kuenea kwa magonjwa haya huzidisha unyanyapaa, ubaguzi na kutengwa kijamii. Watu wanaoishi na NTDs sugu hupata viwango vya juu zaidi vya msongo wa mawazo, wasiwasi na hulka za kujiua ikilinganishwa na jamii kwa ujumla na hata wale wanaoishi na magonjwa mengine sugu. Hata hivyo, wengi wao hawapati huduma na msaada wanaouhitaji ndani ya jamii zao.
“Mapambano dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika si mapambano dhidi ya vijidudu pekee, bali ni mapambano dhidi ya mateso makubwa ya kibinadamu yanayosababishwa na magonjwa haya. Kuyatotokemza kunamaanisha kuwaweka huru watu si tu dhidi ya ugonjwa, bali pia dhidi ya aibu, kutengwa na kukata tamaa ambavyo mara nyingi huambatana nayo.” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa WHO.
Mwongozo wa kwanza wa kimataifa wa kukabiliana na afya ya akili na unyanyapaa
Ili kukabiliana na pengo hili muhimu, WHO hivi karibuni imezindua mwongozo wake wa kwanza wa kimataifa kuhusu Kifurushi Muhimu cha Huduma ECP kwa ajili ya kushughulikia afya ya akili na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na magonjwa ya NTDs.
Mwongozo huo unawapa viongozi wa huduma za afya muhtasari wa hatua zinazotegemea ushahidi kwa ajili ya:
- kukuza afya njema ya akili,
- kutambua na kutathmini matatizo ya afya ya akili kwa watu wanaoishi na NTDs
- kudhibiti na kutibu matatizo ya afya ya akili
- kupunguza unyanyapaa katika ngazi ya mtu binafsi, jamii na mifumo ya afya.
Mafanikio yako hatarini kwa kupungua kwa ufadhili
Kampeni ya kimataifa ya Siku ya NTDs Duniani, inayoongozwa na WHO kwa kushirikiana na muungano wa washirika, inasisitiza kuwa magonjwa ya NTDs bado ni miongoni mwa changamoto rahisi zaidi kutatuliwa na uwekezaji wenye faida kubwa zaidi katika afya ya dunia.
Maendeleo ya muongo uliopita yanaonesha nguvu ya umoja na ushirikiano, idadi ya watu wanaohitaji huduma za NTDs imepungua hadi kiwango cha kihistoria cha watu bilioni 1.4, sambamba na kupungua kwa vifo, madhara ya magonjwa na idadi ya watu walioathiriwa.
Hadi sasa, nchi 58 zimefanikiwa kutokomeza angalau ugonjwa mmoja wa NTDs, jambo linaloiweka dunia kwenye mwelekeo mzuri wa kufikia lengo la WHO la nchi 100 kufikia mwaka 2030.
Kwa mujibu wa WHO nchi kuanzia Brazil hadi Jordan, na kutoka Niger hadi Fiji, zimeonesha kuwa kutokomeza magonjwa haya kunawezekana na ni jambo linaloweza kufikiwa.
Hata hivyo, ripoti ya dunia ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika ya mwaka 2025 inaonesha kuwa msaada rasmi wa maendeleo ODA, kwa ajili ya NTDs umepungua kwa asilimia 41 kati ya mwaka 2018 na 2023, hali inayotishia kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa juhudi kubwa.
Kupungua huku kunatofautiana sana na hoja ya kiuchumi ya kuwekeza katika mapambano dhidi ya NTDs, kila dola moja ya Marekani inayowekezwa katika matibabu ya kinga hutoa faida inayokadiriwa kufikia dola 25.
Bila hatua mpya, NTDs zitaendelea kuathiri maisha na kipato, zikiigharimu familia na jamii zilizoathirika takribani dola bilioni 33 za Marekani kila mwaka kutokana na upotevu wa mishahara na gharama binafsi.
Siku hii ya Magonjwa ya Kitropiki Yaliyosahaulika Duniani ni wito wa kuchukua hatua ili kulinda mafanikio yaliyopatikana, kuhamasisha ufadhili na uongozi mpya, kuharakisha ubunifu, na kuunganisha huduma za afya ikiwemo afya ya akili katika mwitikio wa NTDs.
Kampeni hiyo inahamasisha jumuiya ya kimataifa kuchunguza hadithi za mnepo na mafanikio yanayoongozwa na nchi, yanayoangaziwa kwenye ukurasa wa Siku ya Magonjwa ya Kitropiki Yaliyosahaulika Duniani 2026.