Umoja wa Ulaya umeafikiana kuliorodhesha Jeshi la Mapinduzi la Iran (IRGC) kama kundi la kigaidi, kufuatia ukandamizaji mkali wa maandamano ya kitaifa uliotekelezwa na utawala wa Tehran.
Mkuu wa sera za kigeni wa EU, Kaja Kallas, alisema mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 wanachama walikubaliana kwa kauli moja juu ya uamuzi huo, akisema hatua hiyo inaliweka jeshi hilo “katika daraja moja” na makundi kama al-Qaida, Hamas na IS.
“Wanaotumia ugaidi lazima watendewi kama magaidi,” Kallas alisema.
Maandamano hayo, yaliyochochewa awali na matatizo ya kiuchumi, yaligeuka kuwa changamoto ya moja kwa moja kwa utawala wa kidini wa Iran, kabla ya kukandamizwa kwa nguvu kubwa.
Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu, ukandamizaji huo umeua angalau watu 6,443.
“Utawala wowote unaoua maelfu ya raia wake unaelekea kwenye anguko lake lenyewe,” Kallas aliongeza.
Hatua ya kiishara lakini yenye uzito wa kisiasa
Nchi nyingine kama Marekani na Canada tayari zilishalitaja Jeshi la Mapinduzi la Iran kuwa kundi la kigaidi hapo awali.
Iran pia inakabiliwa na hatari ya hatua za kijeshi za Marekani, kufuatia mauaji ya waandamanaji wasio na silaha na uwezekano wa kunyongwa kwa halaiki.
Jeshi la Marekani tayari limepeleka manowari ya USS Abraham Lincoln pamoja na meli kadhaa za makombora katika eneo la Mashariki ya Kati, ingawa haijulikani kama Rais Donald Trump ataidhinisha matumizi ya nguvu.
Iran, kwa upande wake, ilitoa onyo kwa meli baharini ikisema itafanya mazoezi ya kijeshi yatakayojumuisha matumizi ya risasi hai katika Mlango-Bahari wa Hormuz — njia inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote duniani.
Iran yapuuza uamuzi wa EU
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliupuuza uamuzi huo akiuita “onesho la kisiasa”, na kuonya kuwa Ulaya itaathirika endapo bei za nishati zitapanda kutokana na vikwazo.
“Baadhi ya nchi zinajaribu kuzuia vita kamili katika eneo letu — hakuna hata moja iliyo ya Ulaya,” aliandika kwenye mtandao wa X.
Kristina Kausch, naibu mkurugenzi katika taasisi ya German Marshall Fund, alisema hatua hiyo ni ya kiishara lakini ina ujumbe mzito.
“Inaonyesha kuwa kwa EU, njia ya mazungumzo haijazaa matunda, na sasa kipaumbele ni kuizuia na kuitenga Iran,” alisema.
Aliongeza kuwa kulitaja tawi la kijeshi la serikali kama kundi la kigaidi ni hatua karibu kabisa na kuvunja uhusiano wa kidiplomasia.
Vikwazo vipya na athari za kiuchumi
EU pia imewawekea vikwazo maafisa wakuu 15 wa Iran na taasisi sita, ikiwemo zile zinazohusika na udhibiti wa mtandao, wakati nchi hiyo ikiendelea kuwa katika hali ya kuzimwa kwa intaneti kwa zaidi ya wiki tatu.
Vikwazo hivyo vinajumuisha kufungiwa mali na marufuku ya kusafiri barani Ulaya.
Jeshi la Mapinduzi linadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa Iran, na vikwazo hivyo vinaweza kusababisha mali zake barani Ulaya kutaifishwa.
Iran tayari inasumbuliwa na vikwazo vingi vya kimataifa kutoka Marekani, Uingereza na mataifa mengine.
Jeshi la Mapinduzi: Nguzo ya utawala wa Iran
Jeshi la Mapinduzi lilianzishwa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 kwa lengo la kulinda utawala wa kidini wa Kishia, na baadaye likaingizwa rasmi kwenye Katiba ya Iran.
Lilifanya kazi sambamba na jeshi la kawaida, lakini lilipata nguvu zaidi wakati wa vita vya muda mrefu na Iraq katika miaka ya 1980.
Baada ya vita hivyo, Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei aliliruhusu kupanua shughuli zake katika sekta binafsi, hatua iliyolifanya kuwa na ushawishi mkubwa wa kiuchumi na kisiasa.
Kikosi chake cha Basij kinatajwa kuwa mstari wa mbele katika kukandamiza maandamano, huku video zilizopatikana zikionyesha waandamanaji wakipigwa risasi na kushambuliwa.
Onyo kali la kijeshi na hofu ya vita
Iran imeonya kuwa itajibu “mara moja” endapo itashambuliwa na Marekani.
Msemaji wa jeshi, Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia, alisema kambi za kijeshi za Marekani na hata manowari zinaweza kulengwa.
“Operesheni ya haraka kama anavyofikiria Trump haitatokea,” alionya.
Hatua yoyote ya Iran kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz huenda ikasababisha uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi wa Marekani.
Maafa ya kibinadamu yazidi kuonekana
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema madaktari kadhaa wamekamatwa na wahudumu wa afya kushambuliwa wakiwa wanawahudumia majeruhi.
Hospitali mjini Ilam iliripotiwa kushambuliwa, huku gesi ya machozi ikitumika ndani ya hospitali moja mjini Tehran.
Kwa mujibu wa shirika la Human Rights Activists News Agency, vifo vilivyothibitishwa vinafikia 6,443, huku zaidi ya watu 47,000 wakikamatwa.
Serikali ya Iran, hata hivyo, imetangaza idadi ndogo zaidi ya vifo, ikitaja waliouawa kama “magaidi” — madai ambayo yamekuwa yakitolewa pia katika misukosuko ya awali.
