Madrid, Hispania. Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya England, Jude Bellingham, atakuwa nje ya uwanja kwa takribani mwezi mmoja baada ya kupata majeraha ya nyama ya paja, tukio lililomwacha akitoka uwanjani akiwa analia kwa uchungu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Hispania, Bellingham (22) aliumia mapema kabisa katika ushindi wa mabao 2-1 wa Real Madrid dhidi ya Rayo Vallecano kwenye mchezo wa La Liga uliochezwa jana Jumapili, ambapo alilazimika kutolewa dakika ya 10 baada ya kushindwa kuendelea na mchezo.

Wachezaji wenzake walionekana wakimfariji kiungo huyo. Picha za kabla ya mchezo zilionesha kuwa Bellingham alikuwa tayari anasumbuliwa na maumivu ya msuli kwenye paja la kushoto wakati wa mazoezi ya kupasha misuli kabla ya mechi kuanza lakini bado alianza mchezo.

Kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham akiwa amekaa chini mara baada ya kupata maumivu ya msuli wa paja katika mechi ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ dhidi ya Rayo Valecano. Picha na Mtandao

Baada ya vipimo vya kitabibu kufanyika, Real Madrid imethibitisha kuwa mchezaji huyo amepata majeraha ya misuli kwenye mguu wa kushoto.

“Baada ya vipimo vilivyofanywa leo na idara ya afya ya Real Madrid, Jude Bellingham amegundulika kuwa na jeraha kwenye msuli wa nyama ya paja wa mguu wa kushoto. Tutaendelea kufuatilia maendeleo yake,” ilisema klabu hiyo katika taarifa fupi.

Hata hivyo, gazeti la Marca limeripoti kuwa jeraha hilo linaonekana kuwa kubwa.

Taarifa hizo zimekuja wakati nyota huyo akiwa amekuwa nguzo muhimu ya Real Madrid, akicheza karibu mechi zote tangu alaporejea uwanjani Septemba mwaka jana baada ya kufanyiwa upasuaji wa bega.

Hapo awali, kulikuwa na hofu kuwa jeraha hilo lingeweza kuhatarisha nafasi ya Bellingham kwenye kikosi cha England kuelekea Kombe la Dunia la 2026 litakalofanyika Amerika Kaskazini, ikiwa imebaki miezi minne tu kuanza.

Hata hivyo, kocha wa England, Thomas Tuchel, anaweza kuvuta pumzi baada ya kubainika kuwa kiungo huyo atakaa nje kwa mwezi mmoja tu, huku akitarajiwa kurejea uwanjani mwanzoni mwa Machi endapo hatapata changamoto zaidi.

Jude Bellingham akiwa pamoja na kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel. Picha na Mtandao

Shirikisho la Soka England linaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya afya ya mchezaji huyo, likiwa na wasiwasi juu ya uwezekano wa kukosa muendelezo wa mechi kabla ya michuano hiyo mikubwa, hasa ikizingatiwa umuhimu wake kwenye kikosi cha Taifa cha Simba Watatu.

England imepangwa Kundi L pamoja na Croatia, Ghana na Panama, huku maandalizi ya kuelekea Kombe la Dunia yakitarajiwa kuanza kwa presha kubwa.

Jeraha la Bellingham pia limeibua kumbukumbu za matukio ya nyuma ambapo nyota muhimu wa England walikabiliwa na matatizo ya kiafya kabla ya mashindano makubwa.

Mwaka 2006, aliumia Wayne Rooney kabla ya Kombe la Dunia, jeraha lililomfanya kucheza akiwa hajafikia ubora wake kamili na hatimaye kuondolewa kwa kadi nyekundu katika robo fainali.

Kwa sasa, Real Madrid wanakabiliwa na changamoto ya kukosa huduma ya Bellingham, hususan kwenye mechi ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica.

Klabu hiyo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa La Liga, pointi moja nyuma ya vinara Barcelona, licha ya kushinda mechi zao sita za mwisho za ligi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *