Dar es Salaam . Tangu 2017, jina la Gianluigi Donnarumma (26), halijawa gumzo tu ndani ya viwanja vya soka, pia nje ya uwanja kupitia maisha binafsi hasa uhusiano wake na Alessia Elefante (26), kuanzia kwao Italia.
Wawili hao wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na uhusiano ulioanza bila kelele, lakini baadaye mambo yakabadilika ambapo sasa ni moja ya ‘kapo’ za mastaa wa soka Ulaya zinazojadiliwa sana.
Donnarumma, kipa wa Manchester City kwa sasa na Alessia walianza kuwa pamoja wakiwa bado vijana kipindi ambacho alikuwa anajijenga AC Milan akicheza katika UIwanja wa San Siro.
Uhusiano wao ulianza wakati wote wakiwa na umri wa miaka 17, hivyo wakati Donnarumma akipanda chati ya mafanikio kisoka Alessia alikuwa karibu yake na akisimama kama nguzo muhimu katika maisha yake.
Baada ya takribani miaka miwili ya uhusiano, Alessia aligeuka kutoka kuwa mpenzi wa kawaida na kuwa mchumba wa Donnarumma hatua iliyoashiria dhamira yao ya kujenga maisha ya baadaye pamoja.
Mbali na maisha ya familia, inaelezwa kuwa Alessia ni mbunifu wa ndani wa majengo (interior designer), lakini hapendi sana kujiweka wazi upande huo. Yeye anapenda kupiga picha katika majengo mazuri akiwa mapumziko huko Bahamas au Sardinia.
Alessia ambaye alizaliwa na kukulia nchini Italia hasa jijini Naples ni mtu anayependa sana maisha ya faragha. Ingawa anajulikana kama mchumba wa staa mkubwa wa soka amekuwa akijitahidi kuepuka kelele za mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni Alessia amekuwa akionekana zaidi hadharani hasa kupitia mitandao ya kijamii ambapo ana nguvu ya ushawishi kwa kiasi chake, lakini bado ni mtu anayependa maisha ya faragha. Si miongoni mwa wake au wapenzi wa wachezaji (WAGs) wanaopenda kutafuta umaarufu, bali hupendelea kuishi maisha ya kawaida hata kwenye mitandao.
Kwa sasa ana zaidi ya wafuasi 123,000 kwenye Instagram ambapo mara kwa mara huposti picha za maisha yake na familia, na pia zile anazokuwa uwanjani kumuunga mkono mpenzi wake.
Akiwa uwanjani, mara nyingi huonekana akiwa amevaa jezi au nguo yenye rangi inayofanana na ya timu anayochezea mpenzi wake, jambo linalowafanya mashabiki wengi kumuona kama mwenzao na sio tu mpenzi wa Donnarumma.
Mojawapo wa matukio yaliyogusa hisia za mashabiki ni pale Alessia alipoungana na Donnarumma kusherehekea ushindi wa Paris Saint-Germain (PSG) katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL) 2024/25.
Fainali hiyo iliyopigwa uwanja wa Allianz Arena, ilimalizika kwa PSG kuichapa Inter Milan mabao 5-0, baada ya mchezo huo Donnarumma na Alessia walionekana wakibusiana mbele ya mashabiki, picha iliyosambaa kwa kasi mitandaoni ikionyesha mapenzi yao yalivyo ya dhati. Hata hivyo, maisha yao hayajakosa changamoto kwani Julai 2023, Donnarumma na Alessia walikumbwa na tukio la kushtua baada ya kuvamiwa na kushambuliwa nyumbani jijini Paris.
Tukio hilo lilizua taharuki kubwa, lakini pia liliwaunganisha zaidi likionyesha mshikamano katika nyakati ngumu.
Baada ya kipindi hicho kigumu wapenzi hao walipata furaha kubwa zaidi Septemba 2024 walipojaliwa mtoto wa kwanza wa kiume aliyepewa jina la Leo.
Alessia alitangaza kuzaliwa kwa mtoto huyo kupitia mitandao ya kijamii ambapo aliposti picha wakionekana wakiwa na nyuso za furaha kama wazazi wapya. Muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa Leo, Alessia na Donnarumma waliweka wazi tukio jingine kubwa na muhimu katika maisha yao, ambapo walitangaza rasmi kuchumbiana Oktoba 2024.
Tukio hilo lilipokewa kwa furaha kubwa na mashabiki wao wengi wakieleza kuwa wana matumaini kuwa wawili hao watafunga ndoa siku za usoni. Licha ya tofauti ya urefu kati yao, jambo ambalo limewahi kuzungumziwa sana mitandaoni, hilo halijaonekana kuwa kikwazo katika uhusiano.
Kinyume chake, wawili hao wameendelea kuonyesha mapenzi, heshima na mshikamano wakithibitisha kuwa uhusiano wao umejengwa juu ya misingi imara zaidi ya mwonekano wa nje. Takwimu zinaonyesha kuwa Donnarumma ana urefu wa futi 6 na inchi 5 pamoja na ana uzito wa takribani kilo 90, huku Alessia akiwa na urefu wa futi 5 na inchi 4, na uzito wake ukiwa kilo 55.
Kwa sasa, mashabiki wa Man City wana furaha kumuona Alessia akiwa sehemu yao hasa katika Uwanja wa Etihad ambako wameandika historia kubwa wakiitawala Ligi Kuu England miaka ya karibuni.
Donnarumma anatambulika kama mmoja wa magolikipa bora duniani kwa sasa, licha ya umri wake mdogo, amefanikiwa kuvunja rekodi nyingi na kujijengea heshima kubwa katika soka la kulipwa la kimataifa. Mbali na mafanikio yake uwanjani amejitambulisha pia kama mtu mwenye msimamo usiyoyumba katika maisha yake binafsi. Uhusiano wake na Alessia Elefante umeonekana kuwa wa kudumu, wenye uvumilivu na mshikamano.