KIPA wa Mbeya City, Soud Dondola amesema mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji ni kufa au kupona, akieleza kuwa pointi walizopoteza zinatosha na sasa kazi inaanza upya, huku kocha mkuu Mecky Maxime akisisitiza jambo kwa mastaa wake.

Mbeya City imekuwa na matokeo mabovu tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu, ambapo kwa sasa ipo katika nafasi ya 14 kwa pointi tisa baada ya michezo 12 na leo Jumanne itakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine kuikaribisha Dodoma Jiji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dondola amesema wamepitia kipindi kigumu ambacho kwao wanaona kama sehemu ya kujifunza, akieleza kuwa pointi walizopoteza zinatosha na sasa ni wakati wao kuanza rasmi kazi.

Amesema makosa yaliyoonekana kwa muda wote, benchi la ufundi limeyaona na kuyafanyia kazi akieleza kuwa wataiheshimu Dodoma Jiji, lakini pointi tatu ni lazima ili kurejesha matumaini kwa mashabiki na wao binafsi uwanjani.

“Tumeachana na yaliyotokea nyuma, tunaenda kuanza upya hata maji baharini huchafuka, kisaikolojia tuko fiti na kocha amesahihisha makosa na tumekubaliana na kujifunza kwa kilichojitokeza, ila sasa inatosha na kesho ni kufa au kupona,” amesema Dondola.

Kocha wa timu hiyo, Maxime amesema kumekuwa na tatizo la kuruhusu mabao katika kila mchezo, hali ambayo ameifanyia kazi huku akiwataka mastaa wake kupambana kupata pointi tatu.

Amesema anachofurahia ni jinsi timu ilivyoimarika na kuweza kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini umakini wa kufunga umekuwa changamoto akieleza kuwa anaamini leo kazi itakuwa tofauti.

“Tumekuwa tunaruhusu mabao, lakini nimeliona na kulifanyia kazi, nimewaambia suala la matokeo ya nyuma yasikae akilini bali tupambane upya na bahati nzuri wameimarika kwa kutengeneza nafasi, kilichobaki ni kufunga,” amesema kocha huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *