‘’Mama yangu alikuwa nami lakini watu wengine waliniepuka. Hata niliambiwa nisihudhurie shughuli za familia. Nilihisi kudhalilishwa. Leo, najua ni ugonjwa unaotibika, na ninataka wengine waelewe hilo pia,’’ anasema Tinasoa.
Mzigo huu wa jamii mara nyingi huwakatisha watu tamaa kutafuta ufumbuzi wa mapema au matibabu, na kuruhusu dalili kuwa mbaya zaidi na maambukizi kuongezeka.
Shirika la Afya Duniani lilitenga kila Jumapili ya mwisho wa Januari kuadhimisha Siku ya Ukoma Duniani, sio tu kuashiria maendeleo ya matibabu lakini kukabiliana na majeraha ya kijamii ambayo bado yanaendelea.
Nchi nyingi zimetokomeza kabisa ukoma
Kauli mbiu ya mwaka huu ni; “Ukoma unatibika, changamoto halisi ni unyanyapaa.” Lengo ni kuangazia ukweli uliofichika: wakati sayansi ya matibabu imefanya ugonjwa huo kutibika na kudhibitiwa, hofu, chuki, na kutoelewana vinasalia kuwa vikwazo vikubwa kwa waathirika.
WHO inasema ugonjwa wa ukoma unasalia kuwa tatizo kubwa la afya ya umma, ingawa maendeleo yamepatikana katika miongo kadhaa iliyopita.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni, Mwaka 2023, maambukizi mapya 21,043 ya ukoma yaligunduliwa katika Kanda ya Afrika, ikiwa ni asilimia 11.5 ya jumla ya dunia.
Nchi nyingi zimefanikisha kutokomeza rasmi ukoma kama tatizo la afya ya umma – uliowekwa katika kiwango cha chini cha maambukizi 1 kwa kila watu 10,000 – lakini mifuko ya maambukizi ya juu zaidi imesalia, hasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Madagasca, Msumbiji, Nigeria, na Tanzania.
Unyanyapaa unazuia tiba
Wataalamu wanasisitiza kuwa ingawa viwango vya maambukizi na ugunduzi vinapungua, maambukizi bado yapo, utambuzi wa kuchelewa, na ulemavu unaohusishwa bado unatokea.
Mnamo 2023, jumla ya maambukizi 3,000 ya Ukoma kiwango cha Daraja la 2 – alama ya kuchelewa kugunduliwa – yaliripotiwa barani Afrika.
Tatizo la Ukoma ni kuwa kadri inavyozidi kutokomezwa ndivyo waathirika wanavyozidi kunyanyapaliwa kwa kuonekana wanaugua maradhi ya kale.
Ingawa ukoma ni nadra, bado unaambukiza na hupitishwa kwa njia ya hewa, si kwa kugusa.
Hii inamaanisha kuwa bakteria hupitishwa kupitia matone madogo kutoka kwa pua na mdomo wakati mtu aliyeambukizwa anakohoa au kupiga chafya. Mgusano wa kawaida kama vile kupeana mikono, kukumbatiana, kushiriki chakula, kukaa karibu na mtu, hakuenezi ukoma. Zaidi ya 95% ya watu wana kinga ya asili.
WHO inasema uambukizaji wa Ukoma ni chini hata kuliko magonjwa kama vile TB, COVID-19, au surua na mgonjwa anapoanza matibabu, uwezo wake wa kuambukiza hufifia haraka sana.
Hata hivyo hofu yao ya unyanyapaa inazuia watu wengi kujitokeza kwa ajili ya matibabu, na kusababisha matatizo ya muda mrefu na maambukizi ya ukoma yanayoendelea.