Haya ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Qatar, baada ya maafisa wake kuwa na mazungumzo mjini Doha na yanajiri pia wakati shambulizi la droni likilenga uwanja wa ndege mjini Kisiangani Kaskazini Mashariki mwa Kongo. 

Qatar imesema kundi hilo litapelekwa mjini Uvira, ambao ni mji wa kimkakati Mashariki mwa Kongo, uliodhibitiwa na waasi wa AFC/M23 mwezi Desemba katika mapambano makali, ambako vikosi vya FARDC na washirika wake  waliuteka tena mwezi Januari na kuurudisha chini ya udhibiti wa serikali baada waasi hao kutangaza kuwa wataondoka huko.

Tangazo la kupeleka kikosi cha kulinda amani cha UN mjini humo, lililotolewa jana jioni, ni ishara ya matumaini na hatua ya kusonga mbele katika mazungumzo ya moja kwa moja yaliyosimamiwa na Doha kati ya Congo na waasi hao wa AFC/ M23, ambao mwaka uliopita walifanikiwa kudhibiti maeneo mengi ya Kongo, kuliko walivyowahi kufanya katika siku za nyuma.

Msingi wa ujumbe wa UN na mazungumzo ya Doha

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Qatar imesema serikali ya DRC na waasi wa M23 wamekubaliana tayari kuhusu hatua za kina za kuchukuliwa kwa ufuatiliaji wa njia za usitishaji vita, zilizojadiliwa na kuridhiwa chini ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Oktoba na kuthibitisha kuutekeleza chini ya mpango mkubwa wa amani uliotiwa saini mwezi Novemba.

Msukumo huu wa karibuni wa kufanyia tathmini usitishwaji mapigano hata hivyo, unafanyika wakati mapigano yakiendelea kwenye eneo hilo la Mashariki.

Mwishoni mwa juma serikali ya Kongo ilisema uwanja wa ndege wa Kisiangani ulishambuliwa kwa droni kadhaa Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo.

Maafisa mjini humo wamesema droni nane zilifanikiwa kudunguliwa na hakuna watu wowote waliojeruhiwa au mali kuharibiwa vibaya.

Hapo jana hali ya usalama ilizidi kuimarishwa ndani na nje ya uwanja huo huku operesheni za huko zikiendelea kama kawaida, hii ikiwa ni kulingana na mashuhuda waliozungumza na shirika la habari la AFP kupitia njia ya simu.

Wakaazi Kivu washinikiza kuondolewa MONUSCO DRC

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Iwapo itathibitishwa kwamba M23 ndio waliohusika na shambulizi hilo, itakuwa eneo la mbali ambalo kundi hilo limeanza kushambulia kama sehemu ya vita vyake dhidi ya serikali. Hadi sasa lakini hakuna kundi lolote lililojitokeza kukiri kuhusika na shambulizi hilo.

Mji huo wa Kisiangani ulio na idadi ya watu milioni 1.5 unautegemea pakubwa uwanja wake wa ndege kutokana na hali mbaya ya barabara yake. Uwanja huo wa ndege pia unatumika na jeshi la Kongo kufanyia shughuli zake hasa katika kushambulia ngome za waasi wa M23 kupitia droni na ndege zake za kivita.

Wakati hayo yakiarifiwa Marekani itakuwa mwenyeji wa mazungumzo tofauti kati ya Kongo na Rwanda ambayo Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi wanadai kuwa nchi hiyo inawaunga mkono waasi wa AFC/M23 madai ambayo Rwanda inaendelea kuyakanusha vikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *