
Wachezaji 24 wa Yanga wameondoka leo saa 9 alasiri kuelekea Morocco ambako timu hiyo itakabiliana na FAR Rabat, Jumamosi, Februari 7, 2026 katika mechi ya raundi ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Kundi hilo la wachezaji 24 linahusisha idadi kubwa ya wachezaji wa nafasi ya kiungo jambo ambalo linaashiria wazi kuwa Kocha Mkuu, Pedro Goncalves atakuwa na wigo mpana wa uteuzi katika kiungo.
Wachezaji wa nafasi ya kiungo waliosafiri wako 10 na nafasi inayofuatia kwa kuwa na idadi kubwa ni ya ulinzi ambayo wachezaji wake nane wameenda Morocco.
Ni washambuliaji watatu tu ambao wamesafiri na timu hiyo kwenda Rabat sawa na idadi ya makipa.
Msafara huo unahisisha makipa Djigui Diarra, Hussein Masalanga na Abuutwalib Mshery na mabeki ni Israel Mwenda, Yao Attoula, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Frank Assinki, Dickson Job, Chadrack Boka na Mohamed Hussein.
Viungo ni Aziz Andabwile, Mohamed Damaro, Duke Abuya, Lassine Kouma, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Allan Okello, Edmund John, Pacome Zouzou na Emmanuel Mwanengo.
Washambuliaji watatu ni Depu, Prince Dube na Clement Mzize.
Ili Yanga ifuzu robo fainali, inapaswa kuepuka kufungwa na FAR Rabat katika mchezo huo na kisha ipate ushindi dhidi ya JS Kabylie katika mechi ya mwisho nyumbani.
Ama Yanga inapaswa kutopoteza kwa tofauti ya mabao mawili au zaidi dhidi ya FAR Rabat na kuombea timu hiyo ya Morocco ifungwe na Al Ahly katika mechi ya mwisho.
Matokeo mengine yatakayoibeba Yanga ni kupata ushindi dhidi ya FAR Rabat na kisha sare au ushindi dhidi ya JS Kabylie lakini pia ikiifunga FAR Rabat na kisha JS Kabylie iangushe pointi dhidi ya Ahly.