Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ametangaza leo Ijumaa kwamba “magaidi” wasiopungua 13,000 waliuawa nchini Nigeria mwaka jana, akisisitiza kwamba idadi ya vifo vinavyotokana na uasi wa kutumia silaha nchini humo imepungua kwa 81% tangu alipochukua madaraka Mei 2023.

Tinubu amesisitiza kwamba “zaidi ya magaidi 13,000 waliangamizwa katika mwaka uliopita,” bila kutaja kama anamaanisha 2025 au miezi 12 iliyopita.

Ameongeza kuwa “zaidi ya wapiganaji 124,000 na familia zao wamekabidhi silaha zao tangu 2023 kupitia “Operesheni Njia Salama” (Operation Safe Corridor) iliyoanzishwa na mamlaka ya kuwarekebisha na kuwarejesha uraiani wanamgambo waasi.

Hotuba ya Tinubu imetolewa katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia ya Nigeria, ambayo inaashiria mwisho wa miaka kadhaa ya utawala wa kijeshi na kurejeshwa demokrasia mwaka 1999.

Hata hivyo, licha ya matamshi hayo ya ushindi ya Rais Tinubu, uchumi wa pili kwa ukubwa barani Afrika uko katika hali ngumu ya mgogoro wa ukosefu wa usalama unaozidi kuongezeka ambao umeshuhudia makundi yenye silaha yanayohusiana na ISIL (ISIS) na al-Qaeda, pamoja na magenge ya wahalifu, yakiwateka nyara raia kwa ajili ya kudai pesa za fidia.

Maeneo na vituo vya umma ikiwa ni pamoja na shule, makanisa na misikiti, hasa katika jamii za vijijini zilizo katika mazingira magumu na zenye usalama mdogo, yamekuwa shabaha nyepesi na rahisi za makundi hayo.

Utekaji nyara kwa ajili ya kudai fidia unaongezeka katika maeneo ya kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria, na machafuko yanakaribia kusini magharibi mwa nchi hiyo, ambapo zaidi ya wanafunzi na walimu 40 walitekwa nyara kutoka kwenye shule zao katika Jimbo la Oyo mwezi uliopita wa Mei.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *