“Ombi hili ni wito wa kuungana na watu wanaoishi katika migogoro, waliofurushwa na maafa, ili kuwapa si tu huduma, bali pia kuonesha kuwa dunia haijawapa kisogo,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Ombi la mwaka 2026 lina lengo la kutoa msaada kwa dharura 36 duniani kote, ikiwemo migogoro 14 ya kiwango cha daraja la 3 inayohitaji kiwango cha juu zaidi cha hatua za shirika wakati ufadhili unakokotolewa, kwani ufadhili wa kibinadamu na afya umeshuhudia kupungua kwa kiwango kikali zaidi katika muongo mmoja, limesema shirika hilo.

“Tkriban robo ya watu bilioni wanaishi katika dharura za kibinadamu ambazo zimepoteza usalama, makazi na upatikanaji wa huduma za afya, huku matumizi ya kijeshi duniani yakiwa zaidi ya dola trilioni 2.5 kwa mwaka,” amesema Tedros katika uzinduzi uliofanyika Geneva.

Sio hisani ni muhimu

Kwa rasilimali zinazohitajika, WHO inaweza kudumisha huduma za kuokoa maisha katika dharura mbaya zaidi duniani huku “ikijenga daraja kuelekea amani,” ni shirika kuu la hatua za afya katika mazingira ya kibinadamu, linaloratibu zaidi ya washirika 1,500 katika mazingira 24 ya dharura duniani kote, kuhakikisha mamlaka za kitaifa na washirika wa ndani wanabaki katikati ya jitihada za dharura.

“Sio hisani,” amesema mkuu wa WHO.“Ni uwekezaji wa kimkakati katika afya na usalama, upatikanaji wa huduma za afya unarejesha heshima, unastawisha jamii na unatoa njia kuelekea kujikwamua.”

Maeneo ya kipaumbele kwa hatua za dharura

Kadri ufadhili wa kibinadamu duniani unavyoendelea kupungua, ombi la mwaka 2026 limeibuka katika wakati wa shinikizo za kimataifa zinazoingiliana, kwani migogoro ya muda mrefu, athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoongezeka, na mlipuko wa maradhi yanayojirudia vinazalisha mahitaji makubwa ya msaada wa dharura za afya.

Maeneo ya kipaumbele kwa dharura ya WHO ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Haiti, Myanmar, Eneo la Palestina lililokaliwa kimabavu na Israel, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Syria, Ukraine na Yemen.
Jitihada pia zitashughulikia milipuko inayoendelea ya kipindupindu na mpox.

Kufanya maamuzi magumu

“Ahadi mpya na mshikamano vinahitajika haraka ili kulinda na kusaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi zaidi,” limesema shirika la WHO.

Kwa kuzingatia ufadhili unaopungua, WHO na washirika wengine wa kibinadamu wamekuwa “wakilazimishwa kufanya maamuzi magumu ili kuzingatia uingiliaji muhimu zaidi, limesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa, likiongeza kuwa kile kilichobaki ni shughuli zenye athari kubwa chanya, zikiwemo:

  • kudumisha vituo muhimu vya afya kuhakikisha vikifanya kazi
  • kutoa vifaa vya dharura vya matibabu na huduma za majeraha
  • kuzuia na kukabiliana na milipuko
  • kurejesha chanjo za kawaida
  • kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya ya ngono na uzazi, huduma za mama na mtoto katika mazingira magumu na yaliyoathirika na migogoro.

Huduma za dharura kuwafikia mamilioni

Uwekezaji wa mapema na unaotarajiwa unawezesha WHO na washirika kujibu mara moja pale dharura zinapojitokeza, kupunguza vifo na magonjwa, kudhibiti milipuko na kuzuia hatari za kiafya kuzidi kuwa dharura kubwa za kibinadamu na usalama wa afya zenye gharama kubwa za kibinadamu na kifedha, limesema shirika hilo.

Mwaka 2025, WHO na washirika wake walisaidia watu milioni 30 kwa msaada wa ombi la dharura la kila mwaka. Rasilimali hizi ziliwasaidia:

  • kutoa chanjo za kuokoa maisha kwa watoto milioni 5.3
  • kuwezesha ushauri wa afya kwa watu milioni 53
  • kusaidia zaidi ya vituo vya afya 8,000
  • kuratibu usafirishaji wa kliniki za simu 1,370

Mwaka uliopita, ufadhili wa kibinadamu ulipungua chini ya kiwango cha mwaka 2016, na kuacha WHO na washirika wake wakiwa na uwezo wa kuwafikia tu robo tatu ya watu milioni 81 waliokusudiwa awali kupata msaada wa afya wa kibinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *