Timu ya kisiasa ya Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, imefichua kwamba mauaji yake yamefanywa na watu wanne wasiojulikana waliokuwa na silaha, ambao walivamia nyumba yake katika mji wa Zintan (kilomita 200 kusini-magharibi mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli) alasiri ya jana Jumanne.
Hayo yamesemwa katika taarifa iliyotolewa na timu ya kisiasa ya Saif al-Islam, na kuchapishwa na Abdullah Othman Gaddafi, ambaye ni binamu wa Seif na mwanachama wa timu yake ya kisiasa, kupitia ukurasa wake wa Facebook, akiyataja mauaji hayo kuwa yamefanywa na “mikono ya dhambi.”
Timu hiyo imeongeza kuwa wanaume wanne “wasaliti” waliokuwa wamevalia barakoa walivamia makazi ya Saif al-Islam Gaddafi na kuzima kamera, “katika jaribio la kuficha uhalifu wao” na kwamba Saif al Islam alipambana nao moja kwa moja kabla ya kuuawa.
Kwa upande wake, wakili Mfaransa wa Gaddafi, Marcel Ceccaldi, amesema mauaji ya Saif al-Islam yamefanywa na “kundi la makomandoo lililokuwa na wanajeshi 4” nyumbani kwake katika mji wa Zintan.
Wakati huo huo Kikosi cha 444 cha Libya, kinachoshirikiana na Wizara ya Ulinzi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake makuu Tripoli, kimekana kuwa na uhusiano wowote na mauaji ya Saif al-Islam Gaddafi, na kutangaza kwamba “hakina” uhusiano wowote na mapigano yaliyotokea katika mji wa Zintan na mambo yote yaliyoambatana na mauaji ya Gaddafi.
Taarifa ya kikosi hicho imesema kwamba hakuna maagizo rasmi yaliyotolewa kuhusu kumfuatilia Saif al-Islam Gaddafi, ikisisitiza kwamba jambo hili halikuwa ndani ya majukumu ya “usalama na kijeshi” ya kikosi hicho.
Vilevile kakuna chombo cha serikali au cha mahakama cha mashariki na kusini mwa Libya kilichotoa maelezo yoyote kuhusu mazingira ya kifo cha Saif al-Islam, hasa kwa vile mahali alipokuwa akiishi hapakujulikana hadi kifo chake kilipotangazwa.

Inafaa kuzingatiwa kwamba Saif al-Islam (aliyekuwa na umri wa miaka 53) ni mmoja wa wana wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, na kwa muda mrefu alitambuliwa kuwa mrithi wa baba yake kabla ya kuanguka utawala huo mwaka wa 2011.
Saif al-Islam alifikishwa mbele ya mahakama ya Libya kati ya 2012 na 2013, na akahukumiwa kifo mwaka 2015 kwa tuhuma za mauaji ya halaiki na kuwakandamiza waandamanaji walioshiki katika mapinduzi ya Libya. Pia alikuwa akitafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kuna hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake kupitia Polisii ya Kimataifa (Interpol).