Mbeya. Wanafunzi kutoka vyuo vikuu vitano mkoani Mbeya wanatarajiwa kushiriki mashindano ya ubunifu yatakayolenga kutangaza vivutio zaidi ya 300 vya utalii vilivyopo mkoani humo kupitia makala, picha na video za kidijitali.
Mashindano hayo ni sehemu ya uzinduzi wa Programu ya University Tourism Tour (UTT) iliyoanzishwa na Taasisi ya Ticon kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, ikiwa na lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kutumia ubunifu na teknolojia kutangaza utalii wa ndani na kuvutia wawekezaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Juni 12, 2026, Katibu wa Ticon, Livvet Japhet amesema tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo zimebaini kuwa Mkoa wa Mbeya una vivutio zaidi ya 300 vyenye uwezo mkubwa wa kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii.
Japhet amesema washiriki watatakiwa kuandaa simulizi, makala, picha na video zinazo onyesha historia, utamaduni, mazingira na vivutio mbalimbali vya utalii, ambapo kazi bora zitashindanishwa.
“Tunataka vijana wawe wasimulizi wa hadithi za Tanzania kupitia ubunifu wao badala ya kusimuliwa na watu wengine. Tunawapa nafasi ya kutumia elimu na vipaji vyao kuitangaza nchi,” amesema Katibu huyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Ofisa Maliasili na Mazingira, Annamary Joseph, akizungumza kuhusu manufaa ya Programu ya University Tourism Tour (UTT) kwa Mkoa wa Mbeya wakati wa mkutano na waandishi wa habari. Picha na Hawa Mathias
Amebainisha kuwa washiriki watakaofanya vizuri watawezeshwa kifedha kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii ili kuandaa maudhui yatakayoshindanishwa na kutangazwa kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali.
Vyuo vitakavyoshiriki katika hatua ya awali ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mzumbe (CUoM), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Teofilo Kisanji (TEKU) na Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya.
Japhet amesema matumizi ya teknolojia na mitandao ya kijamii miongoni mwa vijana ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania duniani na kuongeza idadi ya watalii pamoja na wawekezaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ticon, Amani George, amesema programu hiyo inalenga kuhakikisha vivutio vya utalii vinatangazwa, vinalindwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Hii ni programu inayowapa wanafunzi nafasi ya kutumia elimu, ubunifu na teknolojia kuandaa makala, habari, picha na video zitakazoiweka Tanzania kwenye ramani ya utalii duniani,” amesema.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya, Fanuel Munga amesema wanafunzi wako tayari kutumia maarifa na ubunifu wao kutangaza historia, utamaduni na vivutio vya Taifa.
“Kwa niaba ya wanafunzi, tunawahakikishia wadau kuwa tutashiriki kikamilifu katika kutengeneza maudhui yatakayosaidia kuitangaza Tanzania na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya utalii,” amesema.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya na Mkuu wa Kitengo cha Maliasili, Utalii na Mazingira, Annamary Joseph, amesema programu hiyo itaibua vivutio vingi ambavyo havijafahamika na hivyo kuongeza fursa za uwekezaji na mapato ya Serikali.
“Tunaamini kupitia programu hii, Mbeya itanufaika kwa kutangazwa zaidi duniani, jambo litakaloongeza idadi ya watalii na wawekezaji pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla,” amesema.
Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia ubunifu wao kwa uzalendo ili kutangaza utalii wa Tanzania na kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo kupitia maudhui ya kidijitali.