Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limethibitisha katika ripoti yake ya kila mwaka iliyotolewa leo Jumatano kwamba katika mwaka mzima wa 2025 Israel ilifanya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, vitendo vya mauaji ya kimbari na maangamizii ya kizazi dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, na kusababisha vifo, majeraha na kuhamishwa kwa lazima mamia ya maelfu ya watu, kwa kushirikiana na Marekani.

Katika ripoti ya hali ya haki za binadamu katika zaidi ya nchi 100 mwaka jana, shirika hilo limesisitiza kwamba uhalifu wa Israel mwaka 2025 ulifanyika kwa kiwango “ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya hivi karibuni ya Israel na Palestina.”

Katika Ukanda wa Gaza, baada ya jeshi la Israel kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano mnamo Machi 18, 2025, ambayo yalianza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka, Israel iliua zaidi ya Wapalestina 13,500 hadi Oktoba mwaka jana, wakati makubaliano ya pili ya kusitisha mapigano yalipoanza, kwa mujibu na Wizara ya Afya katika ukanda huo.

Hata hivyo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lenye makao yake makuu huko New York City nchini Marekani limesema katika “Ripoti yake ya Mwaka ya 2026” kwamba idadi ya Wapalestina waliouawa mwaka jana kutokana na uhalifu wa Israel ni kubwa kuliko makadirio ya Wizara ya Afya ya Gaza, hasa kwa vile takwimu zake za waliouawa hazijumuishi wale waliozikwa chini ya vifusi au wale waliokufa kutokana na magonjwa, njaa na kiu.

Ripoti ya Human Rights Watch inasema: Uhalifu wa Israel katika Ukanda wa Gaza mwaka jana ulijumuisha mzingiro wa miezi 11, ambapo utawala vamizi wa Israel ulizuia kuingia msaada ya chakula na kusababisha njaa kubwa katika Jiji la Gaza na maeneo ya kandokando yake, vifo vya mamia ya watu kutokana na njaa, pamoja na mauaji ya mamia wakati walipopigwa risasi na mabomu na jeshi la Israel wakisubiri msaada wa kibinadamu kutoka kwa kile kilichojulikana kama “Shirika la Masuala ya Kibinadamu la Gaza,” (Gaza Humanitarian Foundation).

Katika mwaka uliopita, Israel iliendelea kuwakatia umeme na maji wakazi wa Ukanda wa Gaza, na kuzuia kuingia kwa mafuta na kushambulia wafanyakazi na maghala ya nishati.

Human Rights Watch inasema kwamba hatua ya Israel ya kuwanyima maji Wapalestina wa Gaza ni uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mfumo wa mauaji ya kimbari, kwa sababu imesababisha janga kubwa la kiafya miongoni mwa Wapalestina wanaoishi katika kambi zilizojaa watu wengi bila kupata mahitaji ya msingi.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu linasisitiza kwamba hatua ya Israel ya kuwahamisha maelfu ya watu kwa nguvu kutoka Jiji la Gazai Septemba mwaka jana ni sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Human Rights Watch imeutaja uharibifu uliofanywa na jeshi la Israel wa takriban 80% ya majengo ya Gaza, pamoja na uharibifu wa karibu shule zote za ukanda huo, kuwa sawa na maangamizi ya kizazi, kwa sababu ulilifanya eneo hiilo kuwa mahali pasipoweza kuishi watu.

Gaza

Shirika hilo pia limesema kwamba kuwalenga kwa makusudi waandishi wa habari, madaktari na wahudumu wa afya ni miongoni mwa uhalifu ambao utawala wa Israel unaendelea kuufanya, pamoja na kulipua vituo vya afya, hospitali na magari ya wagonjwa.

Shirika la Human Rights Watch limesema kwamba uhalifu wote wa Israel dhidi ya Wapalestina umefanyika kwa ushirikiano wa Marekani, na kuongeza kwamba utawala wa Rais Donald Trump umesaidia na kuunga mkono uhalifu wa kivita wa Israel na kuchukua hatua zilizoifanya Washington kuwa mshiriki katika mzozo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *