
Vyombo vya habari vya kimataifa viimefichua uhusiano unaokua kati ya utawala haramu wa Israel na mrengo wa kulia barani Ulaya, hasa katika kupiga vita Uislamu na Waislamu katika nchi za bara hilo.
Uchambuzi ulioandikwa katika jarida la Foreign Policy, unasema kwamba uhusiano wa Israel na baadhi ya vyama vya mrengo wa kulia vya Ulaya unatokana na muungano wa itikadi na mahesabu za kisiasa, licha ya baadhi ya vyama hivyo kuhusishwa na chuki dhidi ya Wayahudi.
Uchambuzi huo unaonyesha kwamba serikali ya Benjamin Netanyahu – ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa tuhuma za mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita, “imepata katika vyama hivyo chanzo cha uungwaji mkono wa kisiasa katika kukabiliana na taasisi za kimataifa na ukosoaji unaoongezeka wa vita vya mauaji ya kimbari ya watu wa Ukanda wa Gaza, hata kama suala hilo lisababisha mvutano na jamii za Wayahudi barani Ulaya.”
Jarida la Foreign Policy limeandika kuwa, mwelekeo huu unakuja katika muktadha wa mabadiliko katika siasa za Israel kuelekea mrengo wa kulia, sambamba na msisitizo wa pamoja wa kushambulia Uislamu na uhamiaji barani Ulaya, “ambao viongozi wa Israel wanaona kuwa sababu kuu ya kupungua kwa misaada ya Ulaya kwa Tel Aviv katika miaka ya hivi karibuni.”
Mwezi Disemba mwaka jana ripoti mpya ya Shirika la Haki za Kimsingi la Umoja wa Ulaya (FRA) ilifichua sura isiyo ya kawaida ya kuenea chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya.
Ripoti mpya ya shirika la hilo la FRA inaonesha kwamba ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu si ubaguzi tena wa mtu mmoja mmoja au hatua za pembeni zisizo na taathira yoyote bali hivi sasa unyanyasaji huo umekuwa ni sehemu ya miundo ya kitaasisi, kisiasa na vyombo vya habari vya Ulaya.
Kwa mujibu wa shirika hilo Haki za Kimsingi za wakazi wa bara la Ulaya, hotuba za chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu mwaka wa 2025 zilifikia kiwango cha juu mno kuliko wakati wowote katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya zinaanzia mitaani na kwenye mitandao hadi mahali pa kazi na taasisi za elimu.