Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, wamesifu ushirikiano thabiti wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama kati ya nchi hizo mbili wakisema unatuliza hali katika nyakati hizi za mabadiliko na misukosuko duniani.

Xi na Putin wameyasema hayo wakati walipozungumza hii leo kwa njia ya video. Mazungumzo hayo yamefanyika siku chache baada ya maafisa waandamizi kutoka nchi zote mbili kukubaliana kwamba uhusiano wao, unaweza kufungua ukurasa mpya mwaka huu wakati Moscow na Beijing zikiongeza ushirikiano wa kiuchumi.

Xi amemueleza Putin kwamba, tangu mwanzo wa mwaka huu, hali ya kimataifa imeendelea kuwa ya misukosuko zaidi, na kuongeza kuwa nchi zote mbili lazima ziimarishe ushirikiano wao katika mwelekeo sahihi.

Urusi na China zimejaribu kuonyesha mshikamano dhidi ya mataifa ya Magharibi, tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *