Watu wenye silaha wamewaua karibu watu 200 magharibi na kaskazini mwa Nigeria. Hayo yameelezwa na maafisa wa serikali na wakazi wa maeneo hayo huku manusura wakiwazika wenzao waliouawa na askari wa vikosi vya usalama wakiwasaka washambuliaji.

Kwa mujibu wa mbunge wa jimbo la magharibi la Kwara, Saidu Baba Ahmed, watu wenye silaha waliivamia jamii ya Woro Jumanne jioni, na kuwaua watu wasiopungua 170.

Ahmed amevieleza vyombo vya habari kwamba watu hao wenye silaha waliwakamata wakazi, wakawafunga mikono yao nyuma ya migongo yao na kuwaua.

Ameongeza kuwa, wakati wa shambulio hilo, wanakijiji wengine walikimbilia kwenye vichaka vya kandokando, huku washambuliaji wakiendelea kuchoma nyumba na maduka.

Wakati huohuo, wakazi wa jimbo la Katsina lililoko kaskazini ya Nigeria wamesema, watu wasiopungua 21 waliuawa kwa kupigwa risasi na washambuliaji waliowaandama walengwa kutoka nyumba hadi nyumba.

Mauaji ya huko Kwara ni shambulio baya zaidi kufanyika kwenye eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni.

Hayo yanajiri huku wingu la hali mbaya na tata ya kiusalama likiwa limeigubika Nigeria, kuanzia machafuko yanayofanywa na makundi yanayohusishwa na Boko Haram na ISIL (ISIS) kaskazini mashariki, sambamba na ongezeko la utekaji nyara unaofanywa kwa lengo la kudai fidia uanoafanywa na wabeba silaha katika maeneo ya kaskazini magharibi na kaskazini-kati, ambao umeshamiri katika miezi ya hivi karibuni.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio la Kwara.

Wakati huo huo, huko Katsina, wakazi na polisi walisema watu wenye silaha waliwaua watu wasiopungua 21, wakiingia nyumba hadi nyumba kuwapiga risasi raia hao.

Shambulio hilo limeelezewa kwamba, liimevunja mkataba wa amani wa miezi sita uliokuwa umefikiwa kati ya jamii ya eneo hilo na genge la wabeba silaha.

Aidha, limeakisia tatizo kubwa la kiusalama linalowakabili wakazi katika eneo hilo la mbali la kaskazini mwa Nigeria, ambapo baadhi yao wametafuta amani kwa kufikia mwafaka na magenge ya wabeba silaha yanayotoa vitisho dhidi yao. Kwa kawaida, wakazi hao hukusanya pesa na chakula, ambavyo huwapatia majambazi hao ili wasisambuliwe.

Kabir Adamu, mchambuzi wa masuala ya kiusalama katika taasisi ya Ushauri wa Kiualama na Kiintelijensia ya Beacon yenye makao yake mjini Abuja amesema hatua zinazochukuliwa na vikosi vya usalama vya Nigeria kwa ajili ya kudhibiti makundi yenye silaha katika eneo lote hilo hazitoshi…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *