Afisa mwandamizi wa serikali ya Ukraine anasema nchi yake haitakubali masharti yasiyofaa, kama vile hatua za upande mmoja za kuondoa wanajeshi kutoka mistari ya mbele, ili kukomesha mapigano na Urusi.
Naibu Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Ukraine, Pavlo Palisa, alizungumza na NHK katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kyiv mnamo Februari 4.
Kuhusu mazungumzo ya amani, Palisa alisema maelewano yanayowezekana yatakuwa ukomo wa mapigano katika mistari ya mbele ya vita ya sasa.
Aliongeza kuwa Ukraine, kama taifa, haitasalimu amri.
Palisa aliashiria kwamba Urusi inapanga kuteka eneo la Donetsk, mashariki mwa Ukraine ifikapo mwishoni mwa Machi au mapema Aprili, lakini mpango huo hautawezekana na vikosi vya Ukraine vitaendelea kukabiliana na mashambulizi.
Pia alibainisha kuwa Urusi imeongeza kwa kiasi kikubwa mashambulizi dhidi ya vituo vya nishati wakati wa baridi kali, na kukosoa vitendo hivi kama vya ugaidi.
Palisa aliomba usaidizi wa kimataifa uendelee, kama vile utoaji wa mifumo ya ulinzi wa makombora, akisema kwamba Urusi inachambua jinsi ulinzi wa anga wa Ukraine unavyofanya kazi na inajaribu kuwa na ufanisi zaidi.