Maelezo haya ni nukta kumi kwa muhtasari, yakijumuisha ufafanuzi na maoni yangu binafsi, yanayolenga kuchangia mjadala unaoendelea kuhusu swali: je, dhahabu inaweza au inafaa kuuzwa? Ufafanuzi huu umeandaliwa kwa lugha iliyorahisishwa ili usomwe na kueleweka na watu wa kawaida.

Msingi wa hoja hizi unatokana na dhana za uchumi wa kifedha, misingi ya sera ya fedha pamoja na usimamizi wa sarafu chini ya uratibu wa mfumo wa kisasa wa Benki Kuu.

1. Akiba ya fedha za kigeni ni nini?

Benki Kuu duniani huhifadhi fedha za kigeni, maarufu kama foreign currency reserves. Kwa mfano wa kawaida, ni sawa na mtu anayehifadhi Dola, Euro au Yen nyumbani kwa matumizi ya baadaye. Katika uchumi wa taifa, fedha hizi huhifadhiwa kwenye akaunti maalumu za Benki Kuu kwa Tanzania, Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Akiba hii ina kanuni, taratibu na matumizi maalumu, na haisimamiwi kiholela.

2. Je, akiba ya fedha za kigeni ni hazina ya Serikali?

Hapana. Akiba ya fedha za kigeni si sawa na hazina ya Serikali (exchequer). Akaunti ya hazina ya Serikali iko chini ya Wizara ya Fedha na hutumika kukusanya mapato ya bajeti na kugharamia matumizi ya Serikali kama mishahara, miradi na madeni ya ndani. Akiba ya fedha za kigeni ina kazi tofauti kabisa na haitumiki moja kwa moja kwa matumizi ya bajeti.

3. Kwa nini Benki Kuu zinahitaji akiba ya fedha za kigeni?

Sababu kuu ni kuwezesha nchi kuagiza bidhaa na kulipia huduma kutoka nje. Mafuta, dawa, mitambo, magari na bidhaa nyingi hulipiwa kwa fedha za kigeni, hususan Dola ya Marekani.

Aidha, akiba hii hutumika katika kusimamia uthabiti wa sarafu ya nchi, kulingana na miongozo ya sera ya fedha.

4. Akiba ya fedha za kigeni inatosha kwa kiwango gani?

Kwa Tanzania, akiba ya fedha za kigeni imekuwa ikifikia takribani Dola za Marekani bilioni 6. Kitaalamu, akiba huchukuliwa kuwa ya kutosha iwapo inaweza kugharamia uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa angalau miezi minne.

Hiki ndicho kipimo kinachotumika kimataifa, na kinarejelewa katika nyaraka za sera ya fedha za BoT.

5. Dhahabu kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni

Kuanzia mwaka 2023, dhahabu imeanza kuwa sehemu rasmi ya akiba ya fedha za kigeni nchini. BoT ilianzisha utaratibu wa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji na wauzaji wa ndani na kuihifadhi kama akiba.

Kabla ya hapo, hakukuwa na takwimu wazi kuhusu akiba ya dhahabu. Hivyo sasa akiba ya taifa iko katika makundi mawili: fedha za kigeni na dhahabu.

6. Je, dhahabu ni hazina ya sarafu?

Katika mfumo wa kifedha wa kisasa wa fiat currency, dhahabu si dhamana ya sarafu. Ni bidhaa tu inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni. Zamani, chini ya mfumo wa Gold Standard, dhahabu ilikuwa msingi wa thamani ya fedha, lakini mfumo huo ulifutwa rasmi mwaka 1945.

7. Kwa nini Benki Kuu zinahifadhi dhahabu?

Dhahabu ni kitunza thamani. Tofauti na fedha za kawaida zinazopungua thamani kutokana na mfumuko wa bei, dhahabu imekuwa na tabia ya kuhifadhi au kuongeza thamani kwa muda mrefu. Ndiyo maana Benki Kuu nyingi duniani huhifadhi sehemu ya akiba yao katika mfumo wa dhahabu.

8. Kazi ya dhahabu katika akiba ya fedha za kigeni

Akiba, iwe ni fedha au dhahabu, si mali isiyoguswa. Hutumika kulingana na mahitaji ya uchumi. Dhahabu inaweza kuuzwa katika masoko ya kimataifa ili kupata Dola za Marekani kwa ajili ya kulipia uagizaji, madeni ya nje, au kusaidia sera ya uthabiti wa sarafu. Kimsingi, dhahabu inafanya kazi sawa na bidhaa nyingine za kuuza nje kama kahawa au chai.

9. Je, kuuza dhahabu ni kuuza hazina ya taifa?

Kwa mtazamo wa kiuchumi, si kweli. Hata hivyo, dhahabu nyingi inayochimbwa nchini tayari husafirishwa nje na makampuni ya kigeni au ipo mikononi mwa watu binafsi. Hazina halisi ya taifa ni migodi yenyewe kiasi cha dhahabu kilichopo ardhini ni kikubwa mno ukilinganisha na kile kinachohifadhiwa na BoT.

10. Uuzaji wa dhahabu kama mbinu mbadala ya sera ya fedha

Uuzaji wa dhahabu unaweza kuwa njia mbadala ya kupata fedha za kigeni. Badala ya kukopa wakati wa uhaba wa Dola ambako huongeza mzigo wa deni na riba nchi inaweza kuuza sehemu ya dhahabu yake na kugharamia mahitaji ya muda mfupi.

Njia hii inaweza kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje na masharti yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *