Ujerumani yataka kuimarisha mahusiano na nchi za GubaUjerumani yataka kuimarisha mahusiano na nchi za Guba

Wajumbe wa Marekani wameyaelezea mazungumzo ya viongozi hao wawili yaliyofanyika mwanzoni mwa ziara ya siku tatu ya Merz iliyoanza jana (04.02.2026), katika eneo la Ghuba, kuwa ya wazi na mepesi yakituwama katika masuala ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi wa mataifa hayo mawili. Mazungumzo yao yaligusia mambo mbalimbali ikiwemo ulinzi, nishati, Akili Mnemba, mvutano uliopo kati ya Iran na Marekani, hali nchini Syria na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Baada ya mazungumzo yao, Merz alielekea Qatar ambako huko alikutana na kiongozi wa taifa hilo Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani na kusisitiza pia umuhimu wa kuimarisha mahusiano kati yao. Ziara yake hiyo imejikita katika kuimarisha ushirikiano wa Ujerumani kwenye eneo hilo la Ghuba la kimkakati na tajiri ili kuimarisha mahusiano ya muda mrefu ya kiusalama, kiuchumi na biashara. Kando na kile Kansela Merz anachokiona kuwa uhusiano unaofifia kati ya Ulaya na Washington, anajaribu kupunguza utegemezi wa Ujerumani kwa nchi kama Marekani na China.

“Ndiyo maana tunataka kutanua mazungumzo ya kimkakati na Riyadh. Pia tunaimarisha mazungumzo haya na Doha na Abu Dhabi. Tunahitaji ushirikiano kama huo zaidi kuliko wakati mwingine wowote wakati ambapo mataifa makubwa yanazidi kuamua muongozo wa kisiasa wa dunia. Tutaweza kuhifadhi na kuimarisha uhuru wetu, usalama wetu, na ustawi wetu kwa muda mrefu, ikiwa tutakuwa na ushirikiano kama huo,” alisema Friedrich Merz.

Picha ya Pamoja I Merz na Abbas Araghchi
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, akiwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araghchi Picha: Metodi Popow, Iranian Supreme Leader’S Office via ZUMA Press Wire/picture-alliance

Katika eneo hilo la Ghuba Ujerumani inayaangalia maslahi yake, upande wa usambazaji wa nishati, hasa mafuta na gesi, ushirikiano wa ulinzi, aliyosema utazifaidisha pande zote. Kansela huyo wa Ujerumani amesema ushirikiano anaousisitiza kwa mataifa ya Ghuba hasa wa ulinzi, ni wa kuhakikisha kuwa dunia inabakia salama akitilia mkazo kuwa dunia itakuwa salama iwapo mataifa hayo yataweza kujilinda yenyewe. Lakini ametahadharisha kuwa Ujerumani haitosafirisha silaha katika mataifa hayo bila uangalizi wa kina.

Ujerumani: Iran iingie katika mazungumzo kwa nia ya kupata suluhu

Merz pia anataka wawekezaji kutoka mataifa tajiri ya Ghuba kuwekeza Ujerumani hali itakayounda nafasi za ajira. Baada ya ziara yake Saudi Arabia na Qatar, Kansela huyo wa Ujerumani ataelekea Umoja wa Falme za Kiarabu.

Merz pia amezungumzia mzozo unaofukuta kati ya Iran na Marekani akiihimiza Jamhuri hiyo ya Kiislamu kuingia katika mazungumzo yanayotarajiwa kuanza kesho Ijumaa nchini Oman kwa nia ya kupata suluhu, akisema kuna hofu ya ongezeko la kitisho cha kijeshi katika kanda ya Mashariki ya Kati. Amesema Iran lazima ikubali kusitisha mpango wake wa nyuklia ili kuepusha vitisho vya kijeshi kwa Israel na kanda nzima.

Kansela huyo wa Ujerumani pia amejibu kauli ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araghchi, aliyeikaripia nchi hiyo baada ya Merz kutishia kuiwekea vikwazo vipya kutokana na mpango wake huo wa nyuklia na namna ilivyoyashughulikia maandamano ya Januari ya kuipinga serikali ambako inadaiwa watu 6000 waliuwawa na wengine zaidi ya 50,000 kukamatwa.

Araghchi, alisema anasikitika kwamba Ujerumani inageuka kuwa mchokozi badala ya kuwa taifa linalopenda maendeleo barani Ulaya akisema anatumai uongozi imara na thabiti utarejea Ujerumani. Merz amesema kauli hizo za Iran zinaonesha ni za wasiwasi na kutojiamini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *