Maonyesho ya kimataifa ya magari yalianza Februari 5 nchini Indonesia, ambako mauzo ya magari ya umeme yanaongezeka kwa kasi na watengenezaji magari wa China wataangaziwa mno wakati wa maonyesho hayo.
Chapa zaidi ya 30 za magari zinashiriki maonyesho hayo, ambako watengenezaji magari wa Japani waliongoza kwa muda mrefu.
Mwaka huu, watengenezaji wa magari wa China wanachangia idadi kubwa zaidi ya chapa. Watengenezaji wa magari wa nchi hiyo wanaongeza juhudi zao za kuuza magari ya umeme ya bei ya chini.
Kampuni ya GAC AION ya China, ambayo inaongeza mauzo yake kwa kasi nchini Indonesia, itatambulisha aina mpya ya gari lake la umeme kwenye maonyesho hayo.
Mauzo ya magari mapya yamekuwa yakishuka nchini Indonesia hivi karibuni. Lakini mauzo ya magari ya umeme yameongezeka kwa takriban mara sita katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Maonyesho hayo ya magari yanaadhimisha uzinduzi wa kwanza wa gari la umeme la kampuni ya Suzuki Motors ya Japani nchini Indonesia.
Watengenezaji magari wa Japani kwa muda mrefu walikuwa wanashika zaidi ya asilimia 90 ya soko nchini Indonesia. Lakini hii ilishuka hadi takriban asilimia 80 mwaka jana, huku hisa ya mauzo ya magari mapya ya China ikipanda zaidi ya asilimia 10.